Mwanzo 29:1-14
Mwanzo 29:1-14 SRUV
Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki. Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima. Makundi yote hukusanyika huko, watu wakabingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake. Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, ninyi ni watu wa wapi? Wakasema, Sisi tu wa Harani. Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua. Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo. Akasema, Tazama, kungali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha. Wakasema, Hatuwezi, Mpaka makundi yote yakusanyike, watu wakabingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo. Na alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo wa baba yake, maana aliwachunga. Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulibingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye. Yakobo akambusu Raheli, akalia kwa sauti. Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari. Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote. Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.