Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwa 29:1-14

Mwa 29:1-14 SUV

Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki. Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima. Makundi yote hukusanyika huko, watu wakafingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake. Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, watu wa wapi ninyi? Wakasema, Tu wa Harani sisi. Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua. Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo. Akasema, Tazama, ukali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha. Wakasema, Hatuwezi, hata yakusanyike makundi yote, watu wakafingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo. Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga. Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye. Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia. Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari. Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote. Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.