Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 29:1-14

Mwanzo 29:1-14 NEN

Kisha Yakobo akaendelea na safari yake na akafika kwenye nchi za mataifa ya mashariki. Huko akaona kisima katika shamba, pamoja na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu na kisima hicho kwa sababu walikuwa wanakunywa maji kutoka kwenye kisimani hicho. Jiwe lililokuwa mdomoni mwa kisima lilikuwa kubwa. Wakati kondoo wanapokuwa wamekusanyika hapo, wachungaji huvingirisha jiwe hilo kutoka kwenye mdomo wa kisima na kunywesha kondoo. Kisha hulirudisha jiwe mahali pake juu ya mdomo wa kisima. Yakobo aliwauliza wachungaji, “Ndugu zangu, ninyi mmetoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka Harani.” Aliwaambia, “Je, mnamjua Labani, mjukuu wa Nahori?” Wakamjibu, “Ndiyo, tunamfahamu.” Kisha Yakobo akawauliza, “Je, yeye ni mzima?” Wakasema, “Ndiyo, ni mzima, na hapa yuaja Raheli binti yake akiwa na kondoo.” Akasema, “Tazama, jua bado liko juu, si wakati wa kukusanya mifugo. Nywesheni kondoo na mwarudishe malishoni.” Walijibu, “Haiwezekani, mpaka kondoo wote wakusanyike na jiwe liwe limevingirishwa kutoka mdomo wa kisima. Ndipo tutanywesha kondoo.” Alipokuwa akizungumza nao, Raheli akaja pamoja na kondoo wa baba yake, kwa maana alikuwa mchunga kondoo. Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mama yake, pamoja na kondoo wa Labani, alikwenda na kulivingirisha jiwe kutoka mdomoni mwa kisima na kuwanywesha kondoo wa mjomba wake. Kisha Yakobo akambusu Raheli na akaanza kulia kwa sauti. Yakobo alikuwa amemwambia Raheli kuwa yeye alikuwa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Basi Raheli alikimbia na kumweleza baba yake. Mara Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo, mwana wa ndugu yake, aliharakisha kwenda kumlaki. Akamkumbatia na kumbusu, halafu akamleta nyumbani kwake, kisha Yakobo akamwambia mambo yote. Ndipo Labani akamwambia, “Wewe ni nyama yangu na damu yangu mwenyewe.”