Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 21:1-21

Mwanzo 21:1-21 SRUV

BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Abrahamu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Abrahamu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Abrahamu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka mia moja, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, Ni nani angemwambia Abrahamu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Abrahamu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Abrahamu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Abrahamu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Abrahamu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Abrahamu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Abrahamu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akamtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yalipoisha katika kiriba, Hajiri akamlaza kijana kichakani. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.

Soma Mwanzo 21

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 21:1-21