Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwa 21:1-21

Mwa 21:1-21 SUV

BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.

Soma Mwa 21

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwa 21:1-21

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha