Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 21:1-21

Mwanzo 21:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi. Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja. Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka. Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa. Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.” Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!” Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa. Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe. Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake. Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka. Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.” Hivyo, asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari na kumtwika begani; akamfukuza pamoja na mwanawe. Hagari akaondoka, akawa anatangatanga nyikani Beer-sheba. Ikawa maji yalipomwishia katika kile kiriba, Hagari akamlaza mwanawe chini ya mti. Naye akaenda kando, akaketi umbali wa kama mita 100 hivi, akisema moyoni mwake, “Heri nisimwone mwanangu akifa.” Na alipokuwa ameketi hapo, mtoto akalia kwa sauti. Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo. Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.” Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake. Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana. Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 21

Mwanzo 21:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Abrahamu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Abrahamu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Abrahamu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka mia moja, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, Ni nani angemwambia Abrahamu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Abrahamu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Abrahamu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Abrahamu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Abrahamu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Abrahamu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Abrahamu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akamtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yalipoisha katika kiriba, Hajiri akamlaza kijana kichakani. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 21

Mwanzo 21:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 21

Mwanzo 21:1-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huu BWANA akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, naye BWANA akamtendea Sara kile alichokuwa ameahidi. Sara akapata mimba, akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, majira yale ya Mungu aliomwahidi. Abrahamu akamwita Isaki yule mwana ambaye Sara alimzalia. Isaki alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru. Abrahamu alikuwa na miaka 100 wakati Isaki mwanawe alipozaliwa. Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.” Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Abrahamu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Tena nimemzalia mwana katika uzee wake.” Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya. Siku hiyo Isaki alipoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa. Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hagari, Mmisri, aliyemzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki, Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mwanamke huyo mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwanangu Isaki.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe. Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana na mtumishi wako wa kike. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaki. Nitamfanya huyu mwana wa mtumishi wako wa kike kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.” Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari. Akaviweka mabegani mwa Hagari, akamwondoa pamoja na kijana. Hagari akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba. Maji yalipokwisha kwenye kiriba, akamwacha kijana chini ya mojawapo ya vichaka. Kisha akajiendea zake akaketi karibu, umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Ikawa alipokuwa ameketi pale karibu, akaanza kulia kwa huzuni. Mungu akamsikia kijana akilia, malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini Hagari? Usiogope, Mungu amesikia kijana analia akiwa amelala pale. Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.” Ndipo Mungu akamfumbua Hagari macho yake naye akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe. Mungu akawa pamoja na huyu kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde. Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akampatia mke kutoka Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 21