Ezekieli 32:17-32
Ezekieli 32:17-32 SRUV
Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la BWANA likanijia kusema, Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni. Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa. Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametolewa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii. Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, wakiwa wameuawa kwa upanga. Ashuru yuko huko, na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, umati wote wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliotisha katika nchi yao walio hai. Elamu yuko huko, na watu wake umati wote, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka wakiwa hawajatahiriwa hadi pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana vitisho vyao vilifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa. Mesheki yuko huko, na Tubali, na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana walitisha katika nchi ya walio hai. Je! Wasilale pamoja na mashujaa wao wasiotahiriwa, walioanguka, walioshuka kuzimu pamoja na silaha zao za vita, ambao wameweka panga zao chini ya vichwa vyao, na maovu yao mifupani mwao? Maana waliwatisha mashujaa katika nchi ya walio hai. Lakini utavunjika kati ya hao wasiotahiriwa, nawe utalala pamoja nao waliouawa kwa upanga. Edomu yuko huko, wafalme wake, na wakuu wake wote, ambao katika uwezo wao wamelazwa pamoja nao waliouawa kwa upanga; watalala pamoja na hao wasiotahiriwa, na pamoja na hao washukao shimoni. Wakuu wa kaskazini wako huko, wote pia, na Wasidoni, wote walioshuka pamoja na hao waliouawa; kwa sababu ya hofu waliyoleta katika uwezo wao wamefedheheka, nao wamelala wakiwa hawajatahiriwa, pamoja nao waliouawa kwa upanga, nao wanachukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Farao atawaona, naye atapata faraja juu ya watu wake umati wote; naam, Farao, jeshi lake lote waliouawa kwa upanga, asema Bwana MUNGU. Kwa maana nimeweka utisho wake katika nchi ya walio hai; naye atalazwa kati yao wasiotahiriwa, pamoja na hao waliouawa kwa upanga; yeye Farao na watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.