Ezekieli 32:17-32
Ezekieli 32:17-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, mwaka wa kumi na mbili tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Waombolezee watu wengi wa Misri. Wapeleke chini kwenye nchi ya wafu pamoja na mataifa mengine yenye nguvu, waende huko pamoja nao washukao chini kwa wafu. Waambie: Nyinyi ni wazuri kuliko nani? Nendeni kuzimu mlazwe pamoja na wasiomjua Mungu! Watu wa Misri wataangamia pamoja na watu waliouawa vitani. Upanga uko tayari kuangamiza Misri pamoja na watu wake wengi. Wakuu wenye nguvu pamoja na wasaidizi wao wakiwa huko shimoni kwa wafu watasema hivi: ‘Wamisri wameshuka chini kwa wafu, wanalala pamoja na watu wasiomjua Mungu, waliouawa vitani.’ “Waashuru wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Wote waliuawa vitani, na makaburi yao yako sehemu za chini kabisa shimoni kwa wafu. Wanajeshi wao wote waliuawa vitani na makaburi yao yamewazunguka. Hapo awali, walipokuwa wanaishi bado, walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. “Waelamu pia wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao waliouawa vitani. Wote hao wasiomjua Mungu walishuka kwenye nchi ya wafu. Walipokuwa wanaishi bado walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Lakini sasa wanabeba aibu yao pamoja na wanaoshuka shimoni kwa wafu. Wamelazwa na jeshi lao miongoni mwa wale waliouawa vitani. Wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wake wote waliouawa vitani na ambao wote hawamjui Mungu. Walipokuwa bado wanaishi walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai, na sasa wako hapo wamejaa aibu pamoja na wale waliouawa vitani. “Watu wa Mesheki na wa Tabali wote wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Watu hao wote wasiomjua Mungu walikufa vitani, watu ambao walipokuwa hai walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Hao wasiomjua Mungu hawakuzikwa pamoja na mashujaa wa kale, ambao walikwenda kuzimu kwa wafu wakiwa na silaha zao, mapanga yao chini ya vichwa vyao na ngao zao juu ya miili yao. Mashujaa hao walipokuwa wanaishi bado walijaza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Basi, nyinyi Wamisri mtaangamizwa na kulazwa miongoni mwa wasiomjua Mungu waliouawa vitani. “Waedomu wako huko pamoja na wafalme wao na wakuu wao wote. Walipokuwa bado hai walikuwa na nguvu sana, lakini sasa wamelazwa kwa wafu pamoja na wasiomjua Mungu waliouawa vitani. “Viongozi wote wa watu wa kaskazini wako huko pia; hata Wasidoni wote walikwenda kujiunga na wafu. Walipokuwa bado wanaishi, walisababisha vitisho kwa nguvu zao, lakini sasa hao wasiomjua Mungu wamelazwa chini kwa aibu pamoja na wale waliouawa vitani. Wanashiriki aibu ya wale walioshuka shimoni kwa wafu. “Farao, atakapowaona hao wote atafarijika kwa ajili ya wingi wa majeshi yake yote; mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nilimfanya Farao aeneze vitisho katika nchi ya walio hai, lakini sasa yeye mwenyewe pamoja na jeshi lake lote watauawa vitani na kulazwa pamoja na wasiomjua Mungu, waliokufa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli 32:17-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la BWANA likanijia kusema, Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni. Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa. Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametolewa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii. Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, wakiwa wameuawa kwa upanga. Ashuru yuko huko, na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, umati wote wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliotisha katika nchi yao walio hai. Elamu yuko huko, na watu wake umati wote, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka wakiwa hawajatahiriwa hadi pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana vitisho vyao vilifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa. Mesheki yuko huko, na Tubali, na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana walitisha katika nchi ya walio hai. Je! Wasilale pamoja na mashujaa wao wasiotahiriwa, walioanguka, walioshuka kuzimu pamoja na silaha zao za vita, ambao wameweka panga zao chini ya vichwa vyao, na maovu yao mifupani mwao? Maana waliwatisha mashujaa katika nchi ya walio hai. Lakini utavunjika kati ya hao wasiotahiriwa, nawe utalala pamoja nao waliouawa kwa upanga. Edomu yuko huko, wafalme wake, na wakuu wake wote, ambao katika uwezo wao wamelazwa pamoja nao waliouawa kwa upanga; watalala pamoja na hao wasiotahiriwa, na pamoja na hao washukao shimoni. Wakuu wa kaskazini wako huko, wote pia, na Wasidoni, wote walioshuka pamoja na hao waliouawa; kwa sababu ya hofu waliyoleta katika uwezo wao wamefedheheka, nao wamelala wakiwa hawajatahiriwa, pamoja nao waliouawa kwa upanga, nao wanachukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Farao atawaona, naye atapata faraja juu ya watu wake umati wote; naam, Farao, jeshi lake lote waliouawa kwa upanga, asema Bwana MUNGU. Kwa maana nimeweka utisho wake katika nchi ya walio hai; naye atalazwa kati yao wasiotahiriwa, pamoja na hao waliouawa kwa upanga; yeye Farao na watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 32:17-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la BWANA likanijia kusema, Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni. Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa. Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametokwa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii. Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, hali wameuawa kwa upanga. Ashuru yuko huko, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, wote jamii wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliofanya utisho katika nchi yao walio hai. Elamu yuko huko, na watu wake wote jamii, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka hali hawana tohara hata pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana maogofyo yao yalifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa. Mesheki yuko huko, na Tubali, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana walifanya utisho wao katika nchi ya walio hai. Je! Wasilale pamoja na mashujaa wao wasiotahiriwa, walioanguka, walioshuka kuzimu pamoja na silaha zao za vita, ambao wameweka panga zao chini ya vichwa vyao, na maovu yao mifupani mwao? Maana waliwatisha mashujaa katika nchi ya walio hai. Lakini utavunjika kati ya hao wasiotahiriwa, nawe utalala pamoja nao waliouawa kwa upanga. Edomu yuko huko, wafalme wake, na wakuu wake wote, ambao katika uwezo wao wamelazwa pamoja nao waliouawa kwa upanga; watalala pamoja na hao wasiotahiriwa, na pamoja na hao washukao shimoni. Wakuu wa kaskazini wako huko, wote pia, na Wasidoni, wote walioshuka pamoja na hao waliouawa; kwa sababu ya utisho walioufanya katika uwezo wao wamefedheheka, nao wamelala hali hawana tohara, pamoja nao waliouawa kwa upanga, nao wanachukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Farao atawaona, naye atapata faraja juu ya watu wake wote jamii; naam, Farao, jeshi lake lote waliouawa kwa upanga, asema Bwana MUNGU. Kwa maana nimeweka utisho wake katika nchi ya walio hai; naye atalazwa kati yao wasiotahiriwa, pamoja na hao waliouawa kwa upanga; yeye Farao na watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 32:17-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, omboleza kwa ajili ya makundi ya Misri na uwatupe Kuzimu, yeye na binti za mataifa yenye nguvu, waende huko pamoja nao wanaoshuka shimoni. Je, ninyi mmekubalika zaidi ya wengine? Shukeni chini! Nanyi mkalazwe pamoja na hao wasiotahiriwa! Wataanguka miongoni mwa wale waliouawa kwa upanga. Upanga umefutwa; mwache aburutwe mbali pamoja na hao watu wake wote. Kutoka Kuzimu viongozi hodari watanena kuhusu Misri pamoja na wale walioungana nao, ‘Wameshuka chini, nao wamelala kimya pamoja na hao wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.’ “Ashuru yuko huko pamoja na jeshi lake lote, amezungukwa na makaburi ya watu wake wote waliouawa, wale wote walioanguka kwa upanga. Makaburi yao yako kwenye kina cha chini cha shimo na jeshi lake limelala kulizunguka kaburi lake. Wote waliokuwa wameeneza hofu kuu katika nchi ya walio hai wameuawa, wameanguka kwa upanga. “Elamu yuko huko, pamoja na makundi yake yote wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote wameuawa, wameanguka kwa upanga. Wote waliokuwa wameeneza hofu katika nchi ya walio hai walishuka Kuzimu bila kutahiriwa. Wanaichukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni. Kitanda kimetandikwa kwa ajili yake miongoni mwa waliouawa, pamoja na makundi yake yote wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote ni watu wasiotahiriwa, wameuawa kwa upanga. Kwa sababu vitisho vyao vilienea katika nchi ya walio hai, wameichukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni, nao wamewekwa miongoni mwa waliouawa. “Mesheki na Tubali wako humo, pamoja na makundi yao wakiwa wameyazunguka makaburi yao. Wote hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga kwa sababu walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Je, hawakulala na mashujaa wengine wasiotahiriwa waliouawa, ambao wameshuka kaburini wakiwa na silaha zao za vita, ambao panga zao ziliwekwa chini ya vichwa vyao na uovu wao juu ya mifupa yao? Adhabu kwa ajili ya dhambi zao ilikuwa juu ya mifupa yao, ingawa vitisho vya mashujaa hawa vilikuwa vimeenea hadi kwenye nchi ya walio hai. “Wewe pia, ee Farao, utavunjwa nawe utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga. “Edomu yuko humo, wafalme wake wote na wakuu wake wote, ambao ijapokuwa wana nguvu, wamelazwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga. Wamelala pamoja na wasiotahiriwa, pamoja na wale wanaoshuka shimoni. “Wakuu wote wa kaskazini na Wasidoni wote wako huko, wameshuka chini pamoja na waliouawa kwa aibu ijapokuwa kuna vitisho vilivyosababishwa na nguvu zao. Wamelala bila kutahiriwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga na kuchukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni. “Farao, yeye pamoja na jeshi lake lote, atakapowaona atafarijiwa kwa ajili ya makundi yake yote, wale waliouawa kwa upanga, asema BWANA Mwenyezi. Ingawa nilimfanya Farao aeneze vitisho vyake katika nchi ya walio hai, Farao pamoja na makundi yake yote watalazwa miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga, asema BWANA Mwenyezi.”