Eze 32:17-32
Eze 32:17-32 SUV
Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la BWANA likanijia kusema, Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni. Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa. Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametokwa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii. Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, hali wameuawa kwa upanga. Ashuru yuko huko, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, wote jamii wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliofanya utisho katika nchi yao walio hai. Elamu yuko huko, na watu wake wote jamii, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka hali hawana tohara hata pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana maogofyo yao yalifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa. Mesheki yuko huko, na Tubali, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana walifanya utisho wao katika nchi ya walio hai. Je! Wasilale pamoja na mashujaa wao wasiotahiriwa, walioanguka, walioshuka kuzimu pamoja na silaha zao za vita, ambao wameweka panga zao chini ya vichwa vyao, na maovu yao mifupani mwao? Maana waliwatisha mashujaa katika nchi ya walio hai. Lakini utavunjika kati ya hao wasiotahiriwa, nawe utalala pamoja nao waliouawa kwa upanga. Edomu yuko huko, wafalme wake, na wakuu wake wote, ambao katika uwezo wao wamelazwa pamoja nao waliouawa kwa upanga; watalala pamoja na hao wasiotahiriwa, na pamoja na hao washukao shimoni. Wakuu wa kaskazini wako huko, wote pia, na Wasidoni, wote walioshuka pamoja na hao waliouawa; kwa sababu ya utisho walioufanya katika uwezo wao wamefedheheka, nao wamelala hali hawana tohara, pamoja nao waliouawa kwa upanga, nao wanachukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni. Farao atawaona, naye atapata faraja juu ya watu wake wote jamii; naam, Farao, jeshi lake lote waliouawa kwa upanga, asema Bwana MUNGU. Kwa maana nimeweka utisho wake katika nchi ya walio hai; naye atalazwa kati yao wasiotahiriwa, pamoja na hao waliouawa kwa upanga; yeye Farao na watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.