Esta 2:12-19
Esta 2:12-19 SRUV
Basi zamu ya kila mwanamwali kuingia kwa mfalme Ahasuero, iliwadia baada ya kutayarishwa kulingana na sheria ya wanawake kwa miezi kumi na miwili; kwa kuwa ndivyo zilivyotimia siku zao za utakaso, miezi sita kwa mafuta ya manemane, na miezi sita kwa manukato na vifaa vya utakaso wa wanawake; mwanamwali huingia hivyo kwa mfalme; kila alichotaka alipewa kwenda nacho kutoka katika nyumba ya wanawake ili kuingia katika nyumba ya mfalme. Huenda jioni, na asubuhi hurudi katika nyumba ya pili ya wanawake, mikononi mwa Shaashgazi, msimamizi wake mfalme, aliyewalinda masuria. Wala haingii tena kwa mfalme, isipokuwa awe amempendeza mfalme, naye akaitwa kwa jina. Wakati ilipowadia zamu yake Esta, binti Abihaili, mjomba wake Mordekai, ambaye alimtwaa kuwa binti yake, ili aingie kwa mfalme, yeye hakutaka kitu, ila vile vilivyoagizwa na Hegai, msimamizi wake mfalme, aliyewalinda wanawake. Naye huyu Esta alikuwa amepata kibali machoni pa wote waliomwona. Basi Esta alipelekwa kwa mfalme Ahasuero, katika nyumba ya kifalme, mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebethi, mwaka wa saba wa kutawala kwake. Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji la kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti. Ndipo mfalme alipowafanyia karamu kubwa wakuu wake wote na watumishi wake, yaani, karamu yake Esta; akafanya msamaha katika majimbo yote, akatoa zawadi kulingana na ukarimu wa mfalme. Basi mabikira walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa akiketi mlangoni pa mfalme.