Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Est 2:12-19

Est 2:12-19 SUV

Basi ilipowadia zamu yake mwanamwali mmojawapo aingie kwa mfalme Ahasuero, hali akiisha kufanyiwa sawasawa na sheria ya wanawake miezi kumi na miwili; yaani, ndivyo zilivyotimia siku zao za utakaso, miezi sita kwa mafuta ya manemane, na miezi sita kwa manukato na vifaa vya utakaso wa wanawake; mwanamwali huingia hivyo kwa mfalme; kila akitakacho hupewa kwenda nacho kutoka katika nyumba ya wanawake ili kuingia katika nyumba ya mfalme. Huenda jioni, na asubuhi hurudi nyumba ya pili ya wanawake, mikononi mwa Shaashgazi, msimamizi wake mfalme, mwenye kuwalinda masuria. Wala haingii tena kwa mfalme, isipokuwa amempendeza mfalme, naye akaitwa kwa jina. Hata ilipowadia zamu yake Esta, binti Abihaili, mjomba wake Mordekai, ambaye alimtwaa kuwa binti yake, ili aingie kwa mfalme, yeye hakutaka kitu, ila vile vilivyoagizwa na Hegai, msimamizi wake mfalme, mwenye kuwalinda wanawake. Naye huyu Esta alikuwa amepata kibali machoni pa wote waliomwona. Basi Esta alipelekwa kwa mfalme Ahasuero, katika nyumba ya kifalme, mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebethi, mwaka wa saba wa kumiliki kwake. Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti. Ndipo mfalme alipowafanyia karamu kubwa maakida wake wote na watumishi wake, yaani, karamu yake Esta; akafanya msamaha katika majimbo yote, akatoa zawadi sawasawa na ukarimu wa mfalme. Basi mabikira walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa akiketi mlangoni pa mfalme.