Esta 2:1-11
Esta 2:1-11 SRUV
Baada ya hayo, hasira yake mfalme Ahasuero ilipotulia, alimkumbuka Vashti, na vile alivyotenda, na yale yaliyoamriwa juu yake. Basi watumishi wa mfalme waliomhudumia walimwambia, Mfalme na atafutiwe mabikira vijana wazuri; naye mfalme aweke wasimamizi katika mikoa yote ya ufalme wake, ili wakusanye pamoja mabikira vijana wazuri wote waende Susa, mji mkuu kwenye nyumba ya wanawake mikononi mwa Hegai, msimamizi wa nyumba ya mfalme, mwenye kuwalinda wanawake; tena wapewe vifaa vya utakaso. Naye yule msichana atakayempendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti. Neno hilo likampendeza mfalme, naye akafanya hivyo. Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Susa, mji mkuu; jina lake Mordekai, mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, wa kabila la Benyamini; ambaye alikuwa amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alimchukua. Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo nzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake. Basi amri ya mfalme na mbiu yake iliposikiwa, wasichana wengi wakakusanyika huko Susa, mji mkuu mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake. Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na chakula chake, na vijakazi saba wa nyumbani mwa mfalme ili wamhudumie. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake. Naye Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe. Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na yale yatakayompata.