Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 2:1-11

Esta 2:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadaye, hasira yake ilipokwisha tulia, mfalme Ahasuero alimkumbuka Vashti, akawa anatafakari juu ya ukaidi wake na hatua iliyochukuliwa dhidi yake. Basi, watumishi wake, waliokuwa wanamhudumia yeye binafsi, wakamshauri, “Kuna wasichana wengi wazuri; kwa nini usitafutiwe mmoja? Unaweza kuteua maofisa katika kila mkoa wa utawala wako, na kuwaagiza wawalete wasichana wazuri wote kwenye nyumba ya wanawake hapa Susa, mji mkuu. Halafu wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wako; na hapo wapewe mafuta na vifaa vingine ili wajirembeshe zaidi. Yule atakayekupendeza zaidi, na afanywe malkia badala ya Vashti.” Mfalme akaona shauri hilo ni jema, akafanya hivyo. Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini. Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni. Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake. Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake. Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie. Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo. Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.

Shirikisha
Soma Esta 2

Esta 2:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Baada ya hayo, hasira yake mfalme Ahasuero ilipotulia, alimkumbuka Vashti, na vile alivyotenda, na yale yaliyoamriwa juu yake. Basi watumishi wa mfalme waliomhudumia walimwambia, Mfalme na atafutiwe mabikira vijana wazuri; naye mfalme aweke wasimamizi katika mikoa yote ya ufalme wake, ili wakusanye pamoja mabikira vijana wazuri wote waende Susa, mji mkuu kwenye nyumba ya wanawake mikononi mwa Hegai, msimamizi wa nyumba ya mfalme, mwenye kuwalinda wanawake; tena wapewe vifaa vya utakaso. Naye yule msichana atakayempendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti. Neno hilo likampendeza mfalme, naye akafanya hivyo. Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Susa, mji mkuu; jina lake Mordekai, mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, wa kabila la Benyamini; ambaye alikuwa amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alimchukua. Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo nzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake. Basi amri ya mfalme na mbiu yake iliposikiwa, wasichana wengi wakakusanyika huko Susa, mji mkuu mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake. Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na chakula chake, na vijakazi saba wa nyumbani mwa mfalme ili wamhudumie. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake. Naye Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe. Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na yale yatakayompata.

Shirikisha
Soma Esta 2

Esta 2:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Baada ya hayo, hasira yake mfalme Ahasuero ilipotulia, alimkumbuka Vashti, na vile alivyotenda, na yale yaliyoamriwa juu yake. Basi watumishi wa mfalme waliomhudumu walimwambia, Mfalme na atafutiwe mabikira vijana wazuri; naye mfalme aweke wasimamizi katika majimbo yote ya ufalme wake, ili wakusanye pamoja mabikira vijana wazuri wote waende Shushani ngomeni, kwenye nyumba ya wanawake mikononi mwa Hegai, msimamizi-wa-nyumba wa mfalme, mwenye kuwalinda wanawake; tena wapewe vifaa vya utakaso. Naye yule msichana atakayempendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti. Neno hilo likampendeza mfalme, naye akafanya hivyo. Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Shushani ngomeni; jina lake Mordekai, bin Yairi, bin Shimei, bin Kishi, wa kabila ya Benyamini; ambaye kwamba amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alimchukua. Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye. Basi ikawa, wakati iliposikiwa amri ya mfalme na mbiu yake, wasichana wengi wakakusanyika huko Shushani ngomeni mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake. Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na posho zake, na vijakazi saba walio haki yake, wa nyumbani mwa mfalme. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake. Walakini Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe. Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na hayo yatakayompata.

Shirikisha
Soma Esta 2

Esta 2:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baadaye, wakati hasira ya Mfalme Ahasuero ilikuwa imetulia, alimkumbuka Vashti na kile alichokuwa amekifanya na alilokuwa ameamuru juu yake. Kisha watumishi waliomhudumia mfalme walipendekeza, “Na ufanyike utafiti kwa ajili ya wanawali mabikira wazuri wa sura kwa ajili ya mfalme. Mfalme na ateue maafisa katika kila jimbo la himaya yake kuwaleta hao wanawali wote wazuri wa sura katika nyumba ya wanawake katika ngome ya mji wa Shushani. Kisha wawekwe chini ya utunzaji wa Hegai, towashi wa mfalme, msimamizi wa wanawake; na wapewe matunzo yote ya urembo. Kisha yule ambaye atampendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti.” Shauri hili likampendeza mfalme, naye akalifuata. Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila ya Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda. Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki. Wakati agizo na amri ya mfalme lilitangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake. Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya uzuri na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake. Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wala kabila lake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza. Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.

Shirikisha
Soma Esta 2