Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Torati 6:4-25

Kumbukumbu la Torati 6:4-25 SRUV

Sikiliza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyasema uishipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako. Kisha BWANA Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Abrahamu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vilivyochimbwa usivyochimba wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. Mche BWANA, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake. Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao; kwani BWANA, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya BWANA, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi. Msimjaribu BWANA, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa. Zishikeni kwa bidii sheria za BWANA, Mungu wenu, na maagizo yake, na amri zake alizokuagiza. Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa BWANA; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri BWANA aliyowaapia baba zako, ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema BWANA. Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, Ni nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza BWANA, Mungu wetu? Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; BWANA, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu; BWANA akaonesha ishara na maajabu makubwa na mazito, juu ya Misri, Farao, na nyumba yake yote, mbele ya macho yetu; akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia babu zetu. BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche BWANA, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo. Tena itakuwa haki kwetu, tukizingatia kufanya maagizo haya yote mbele ya BWANA, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha