Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 6:4-25

Kumbukumbu 6:4-25 NEN

Sikia, ee Israeli: BWANA Mungu wako, BWANA ni mmoja. Mpende BWANA Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako. Wakati BWANA Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Abrahamu, Isaki na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, ina miji inayopendeza ambayo hukuijenga, nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba, jihadhari usije ukamwacha BWANA, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. Utamcha BWANA Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake. Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka; kwa kuwa BWANA Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi. Usimjaribu BWANA Mungu wako kama ulivyofanya huko Masa. Utayashika maagizo ya BWANA Mungu wako kwa bidii, na masharti na amri alizokupa. Fanya lililo haki na jema mbele za BWANA, ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayo BWANA aliahidi kwa kiapo kwa baba zako, kuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kama BWANA alivyosema. Siku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazo BWANA Mungu wako alikuagiza wewe?” Mwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakini BWANA alitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu. BWANA akapeleka mbele yetu ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno juu ya Misri na Farao pamoja na nyumba yake yote. Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupa nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo. BWANA akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha BWANA Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo. Kama tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za BWANA Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha