Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 6:4-25

Kumbukumbu la Sheria 6:4-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako. Tena itakuwa atakapokwisha BWANA, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. Mche BWANA, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake. Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao; kwani BWANA, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya BWANA, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi. Msimjaribu BWANA, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa. Zishikeni kwa bidii sheria za BWANA, Mungu wenu, na mashuhudizo yake, na amri zake alizokuagiza. Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa BWANA; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri BWANA aliyowaapia baba zako, ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema BWANA. Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, N’nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza BWANA, Mungu wetu? Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; BWANA, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu; BWANA akaonya ishara na maajabu, makubwa, mazito, juu ya Misri, na juu ya Farao, na juu ya nyumba yake yote, mbele ya macho yetu; akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia baba zetu. BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche BWANA, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo. Tena itakuwa haki kwetu, tukitunza kufanya maagizo haya yote mbele ya BWANA, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.

Kumbukumbu la Sheria 6:4-25 Biblia Habari Njema (BHN)

“Basi sikilizeni enyi Waisraeli! Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni Mwenyezi-Mungu mmoja. Mpendeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wenu wote, kwa roho yenu yote na kwa nguvu zenu zote. Wekeni mioyoni mwenu maneno hayo ninayowaamuru leo na kuwafundisha kwa uangalifu watoto wenu. Mtawasimulia muwapo mnakaa nyumbani au mlipo safarini au mnapolala au mnapoamka. Yafungeni katika mikono yenu na kuyavaa katika vipaji vya nyuso zenu kama ukumbusho. Yaandikeni kwenye miimo ya milango yenu na malango ya miji yenu. “Kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, yeye atawapeni nchi yenye miji mikubwa na mizuri iliyostawi ambayo nyinyi hamkuijenga. Nyumba zitakuwa zimejaa vitu vizuri ambavyo nyinyi hamkuviweka, kutakuwa na visima ambavyo hamkuvichimba na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuyapanda. Mwenyezi-Mungu atakapowapeleka kwenye nchi hiyo ambako mtakuwa na chakula chote mnachohitaji, hakikisheni kwamba hamtamsahau Mwenyezi-Mungu aliyewatoa Misri ambako mlikuwa watumwa. Mtamcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtamtumikia yeye peke yake na kuapa kwa jina lake peke yake. Msiabudu miungu mingine, miungu ya watu walio jirani nanyi, hasira ya Mwenyezi-Mungu isije ikawaka juu yenu, naye akawafutilia mbali kutoka duniani, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliye kati yenu, ni Mungu mwenye wivu. “Msimjaribu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu kule Masa. Hakikisheni kwamba mnazitii amri zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maamuzi na masharti yake ambayo amewaamuru. Fanyeni yale yanayompendeza Mwenyezi-Mungu, ili mpate kufanikiwa. Mtaweza kuimiliki nchi ile nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu aliapa kuwapa babu zenu, na kwamba Mwenyezi-Mungu atawafukuza adui zenu kama alivyoahidi. “Siku zijazo, watoto wenu wakiwauliza, ‘Nini maana ya maamuzi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, aliwaamuru kutenda?’ Nyinyi mtawajibu hivi: ‘Sisi tulikuwa watumwa wa Farao, mfalme wa Misri, na Mwenyezi-Mungu akatuokoa kwa mkono wake wenye nguvu. Kwa macho yetu wenyewe tulimwona akifanya ishara na miujiza na mambo ya kutisha na ya ajabu dhidi ya Wamisri, mfalme wao na wakuu wake. Alitutoa Misri, akatuleta hapa na kutupa nchi hii, kama alivyoapa kwamba atawapa babu zetu. Basi, Mwenyezi-Mungu alituamuru kuzitii kanuni hizi zote na kumcha kwa faida yetu wenyewe; apate kutulinda daima kama hivi leo. Tena tutakuwa waadilifu kama tukitimiza kwa uangalifu amri hizi zote mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyotuamuru’.

Kumbukumbu la Sheria 6:4-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Sikiliza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyasema uishipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako. Kisha BWANA Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Abrahamu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vilivyochimbwa usivyochimba wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. Mche BWANA, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake. Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao; kwani BWANA, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya BWANA, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi. Msimjaribu BWANA, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa. Zishikeni kwa bidii sheria za BWANA, Mungu wenu, na maagizo yake, na amri zake alizokuagiza. Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa BWANA; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri BWANA aliyowaapia baba zako, ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema BWANA. Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, Ni nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza BWANA, Mungu wetu? Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; BWANA, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu; BWANA akaonesha ishara na maajabu makubwa na mazito, juu ya Misri, Farao, na nyumba yake yote, mbele ya macho yetu; akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia babu zetu. BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche BWANA, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo. Tena itakuwa haki kwetu, tukizingatia kufanya maagizo haya yote mbele ya BWANA, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.

Kumbukumbu la Sheria 6:4-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Sikia, ee Israeli: BWANA Mungu wako, BWANA ni mmoja. Mpende BWANA Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako. Wakati BWANA Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Abrahamu, Isaki na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, ina miji inayopendeza ambayo hukuijenga, nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba, jihadhari usije ukamwacha BWANA, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. Utamcha BWANA Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake. Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka; kwa kuwa BWANA Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi. Usimjaribu BWANA Mungu wako kama ulivyofanya huko Masa. Utayashika maagizo ya BWANA Mungu wako kwa bidii, na masharti na amri alizokupa. Fanya lililo haki na jema mbele za BWANA, ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayo BWANA aliahidi kwa kiapo kwa baba zako, kuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kama BWANA alivyosema. Siku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazo BWANA Mungu wako alikuagiza wewe?” Mwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakini BWANA alitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu. BWANA akapeleka mbele yetu ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno juu ya Misri na Farao pamoja na nyumba yake yote. Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupa nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo. BWANA akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha BWANA Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo. Kama tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za BWANA Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”

Kumbukumbu la Sheria 6:4-25

Kumbukumbu la Sheria 6:4-25 BHNKumbukumbu la Sheria 6:4-25 BHNKumbukumbu la Sheria 6:4-25 BHNKumbukumbu la Sheria 6:4-25 BHNKumbukumbu la Sheria 6:4-25 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha