Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 7:17-36

Matendo 7:17-36 SRUV

Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, hata mfalme mwingine asiyemfahamu Yusufu akaanza kutawala katika Misri. Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi. Wakati huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya babaye. Wakati alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe. Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo. Umri wake ulipokuwa kama miaka arubaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipizia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. Kesho yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa kama mgeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko. Hata miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika muali wa moto, kichakani. Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia, Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama. Bwana akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu. Hakika nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri. Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka. Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika Bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arubaini.

Soma Matendo 7