Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 7:17-36

Matendo 7:17-36 Biblia Habari Njema (BHN)

“Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi. Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri. Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe. Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu, na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea kama mtoto wake. Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo. “Alipokuwa na umri wa miaka arubaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli. Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kwa kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. ( Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo). Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha akisema: ‘Nyinyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya nyinyi kwa nyinyi?’ Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’ Baada ya kusikia hayo, Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili. “Miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai. Mose alistaajabu sana kuona tukio hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana: ‘Mimi ni Mungu wa babu zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!’ Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi. Bwana akamwambia: ‘Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu. Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.’ “Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?’ Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi. Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani, kwa muda wa miaka arubaini.

Shirikisha
Soma Matendo 7

Matendo 7:17-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, hata mfalme mwingine asiyemfahamu Yusufu akaanza kutawala katika Misri. Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi. Wakati huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya babaye. Wakati alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe. Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo. Umri wake ulipokuwa kama miaka arubaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipizia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. Kesho yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa kama mgeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko. Hata miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika muali wa moto, kichakani. Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia, Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama. Bwana akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu. Hakika nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri. Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka. Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika Bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arubaini.

Shirikisha
Soma Matendo 7

Matendo 7:17-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, hata mfalme mwingine akainuka juu ya Misri, asiyemfahamu Yusufu. Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi. Wakati huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya babaye. Hata alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe. Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo. Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko. Hata miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika mwali wa moto, kijitini. Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia, Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama. Bwana akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu. Yakini nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri. Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti. Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini.

Shirikisha
Soma Matendo 7

Matendo 7:17-36 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

“Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Ibrahimu, watu wetu walizidi kuongezeka sana huko Misri. Ndipo ‘mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri’. Huyu mfalme akawatendea watu wetu hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe. “Wakati huo Musa alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani mwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu. Walipomweka nje mtoni, binti Farao akamchukua akamlea kama mtoto wake. Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo. “Musa alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli. Aliona mmoja wao akidhulumiwa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamuua kulipiza kisasi. Musa alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa. Siku iliyofuata Musa aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kudhulumiana?’ “Lakini yule mtu aliyekuwa akimdhulumu mwenzake akamsukuma Musa kando, akamuuliza, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’ Musa aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume. “Baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Musa jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Mwenyezi Mungu, ikisema: ‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’ Musa alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama. “Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu. Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’ “Huyu ndiye Musa waliyemkataa waliposema, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kupitia kwa yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka. Aliwaongoza Waisraeli kutoka Misri baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamu, na katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.

Shirikisha
Soma Matendo 7