Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 7:17-36

Matendo 7:17-36 NENO

“Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Ibrahimu, watu wetu walizidi kuongezeka sana huko Misri. Ndipo ‘mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri’. Huyu mfalme akawatendea watu wetu hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe. “Wakati huo Musa alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani mwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu. Walipomweka nje mtoni, binti Farao akamchukua akamlea kama mtoto wake. Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo. “Musa alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli. Aliona mmoja wao akidhulumiwa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamuua kulipiza kisasi. Musa alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa. Siku iliyofuata Musa aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kudhulumiana?’ “Lakini yule mtu aliyekuwa akimdhulumu mwenzake akamsukuma Musa kando, akamuuliza, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’ Musa aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume. “Baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Musa jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Mwenyezi Mungu, ikisema: ‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’ Musa alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama. “Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu. Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’ “Huyu ndiye Musa waliyemkataa waliposema, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kupitia kwa yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka. Aliwaongoza Waisraeli kutoka Misri baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamu, na katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.