Matendo 19:8-22
Matendo 19:8-22 SRUV
Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa la mtu mmoja, jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wagiriki. Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawatoka, pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwapo wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile wakiwa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wagiriki waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha elfu hamsini. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia. Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kwa muda.