Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 19:8-22

Matendo 19:8-22 NENO

Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao wakakaidi; walikataa kuamini, na wakakashifu Njia Ile hadharani. Basi Paulo aliachana nao. Akaenda na wanafunzi wale, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano. Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko jimbo la Asia wakawa wamesikia neno la Bwana. Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kupitia kwa Paulo, hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi waliotangatanga wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu kwa wale wenye pepo, wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.” Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. Siku moja pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha. Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana. Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma elfu hamsini za fedha. Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu. Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.” Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko jimbo la Asia.

Video ya Matendo 19:8-22