Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 19:8-22

Matendo 19:8-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani. Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia. Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kitambo.

Shirikisha
Soma Matendo 19

Matendo 19:8-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya juu ya hiyo njia ya Bwana katika kusanyiko la watu. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano. Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana. Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: “Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri.” Watoto saba wa Skewa, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu. Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda. Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande 50,000 vya fedha. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi. Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, “Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia.” Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia.

Shirikisha
Soma Matendo 19

Matendo 19:8-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa la mtu mmoja, jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wagiriki. Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawatoka, pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwapo wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile wakiwa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wagiriki waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha elfu hamsini. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia. Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kwa muda.

Shirikisha
Soma Matendo 19

Matendo 19:8-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya Ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao walikaidi. Walikataa kuamini, na wakakashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu. Basi Paulo aliachana nao. Akawachukua wanafunzi naye, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano. Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana. Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo, hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka. Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.” Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha. Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana. Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000 za fedha. Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu. Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.” Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia.

Shirikisha
Soma Matendo 19