Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 12:1-16

Matendo 12:1-16 SRUV

Karibu wakati ule ule, Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi aliendelea na kumshika Petro pia. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakalilinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita kundi la walinzi wa kwanza na wa pili, wakafika hadi mbele ya lango la chuma la kuingilia mjini, nalo lango likawafungukia lenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Ndipo Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua hakika kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakulifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akasisitiza, akasema ya kwamba ndivyo ilivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafululiza kugonga, hadi walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.

Soma Matendo 12