Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 12

12
Yakobo auawa na Petro kufungwa
1 # Mdo 4:3 Karibu wakati ule ule, Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. 2Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. 3Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi aliendelea na kumshika Petro pia. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. 4#Kut 12:1-27 Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu.
5 # Yak 5:16 Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.
Petro akombolewa kutoka Gerezani
6 # Mdo 5:22,23 Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakalilinda gereza. 7#Mdo 5:19 Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. 8Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. 9Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. 10Na walipopita kundi la walinzi wa kwanza na wa pili, wakafika hadi mbele ya lango la chuma la kuingilia mjini, nalo lango likawafungukia lenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. 11Ndipo Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua hakika kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. 12#Mdo 12:25; 15:37 Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. 13Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. 14Alipoitambua sauti ya Petro, hakulifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. 15#Mdo 26:24; Lk 24:37 Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akasisitiza, akasema ya kwamba ndivyo ilivyo. Wakanena, Ni malaika wake. 16Petro akafululiza kugonga, hadi walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu. 17Naye akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza. Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali pengine.
18 # Mdo 5:21,22 Kulipopambazuka askari wakaingiwa na fadhaa juu ya yaliyompata Petro. 19Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwahoji wale walinzi, akaamuru wauawe. Kisha akateremka kutoka Yudea kwenda Kaisaria, akakaa huko.
Kifo cha Herode
20 # 1 Fal 5:9; Eze 27:17 Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulala, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme. 21Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. 22#Eze 28:2 Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya mungu, si sauti ya mwanadamu. 23#Dan 5:20 Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na wadudu, akatokwa na roho.
24 # Mdo 6:7; Isa 55:11 Neno la Bwana likazidi na kuenea.
25 # Mdo 11:29; 12:12; 15:37 Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohana aitwaye Marko.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 12: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia