Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 12:1-16

Matendo 12:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Karibu wakati huohuo, mfalme Herode alianza kuwatesa baadhi ya Wakristo. Alimuua kwa upanga Yakobo, ndugu yake Yohane. Alipoona kuwa kitendo hicho kiliwapendeza Wayahudi, aliendelea, akamkamata Petro. (Hiyo ilifanyika wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu). Baada ya kutiwa nguvuni, Petro alifungwa gerezani, akawekwa chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari wannewanne. Herode alikusudia kumtoa hadharani baada ya sikukuu ya Pasaka. Basi, Petro alipokuwa gerezani, kanisa lilikuwa linamwombea kwa Mungu kwa moyo. Usiku, kabla ya siku ile ambayo Herode angemtoa Petro hadharani, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili. Alikuwa amefungwa minyororo miwili, na walinzi walikuwa wanalinda lango la gereza. Ghafla, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na mwanga ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa ubavuni akamwamsha akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo iliyomfunga mikono ikakatika na kuanguka chini. Malaika akamwambia, “Jifunge mshipi wako, vaa viatu vyako.” Akafanya hivyo. Kisha huyo malaika akamwambia, “Vaa koti lako, unifuate.” Petro akamfuata nje lakini hakujua kama hayo yaliyofanywa na huyo malaika yalikuwa ya kweli; alidhani alikuwa anaota ndoto. Walipita kituo cha kwanza cha ulinzi na cha pili, halafu wakafika kwenye mlango wa chuma wa kuingilia mjini. Huo mlango ukawafungukia wenyewe, nao wakatoka nje. Wakawa wanatembea katika barabara moja na mara yule malaika akamwacha Petro peke yake. Hapo ndipo Petro alipotambua yaliyotukia, akasema, “Sasa najua kwa hakika kwamba Bwana amemtuma malaika wake akaniokoa mikononi mwa Herode na kutoka katika mambo yale yote watu wa Israeli waliyotazamia.” Alipotambua hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Maria mama yake Yohane aitwaye Marko. Humo watu wengi walikuwa wamekusanyika wakisali. Petro alipiga hodi kwenye mlango wa nje na mtumishi mmoja msichana aitwaye Roda, akaenda mlangoni kuitikia. Huyo msichana aliitambua sauti ya Petro akafurahi mno, hata badala ya kuufungua ule mlango, akakimbilia ndani na kuwaambia kwamba Petro alikuwa amesimama nje mlangoni. Wakamwambia yule msichana, “Una wazimu!” Lakini yeye akasisitiza kwamba ilikuwa kweli. Nao wakamwambia, “Huyo ni malaika wake.” Wakati huo Petro alikuwa anaendelea kupiga hodi. Mwishowe walifungua mlango, wakamwona, wakashangaa.

Shirikisha
Soma Matendo 12

Matendo 12:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Karibu wakati ule ule, Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi aliendelea na kumshika Petro pia. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakalilinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita kundi la walinzi wa kwanza na wa pili, wakafika hadi mbele ya lango la chuma la kuingilia mjini, nalo lango likawafungukia lenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Ndipo Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua hakika kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakulifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akasisitiza, akasema ya kwamba ndivyo ilivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafululiza kugonga, hadi walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.

Shirikisha
Soma Matendo 12

Matendo 12:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.

Shirikisha
Soma Matendo 12

Matendo 12:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huo huo Mfalme Herode Agripa aliwakamata baadhi ya watu wa kanisa. Akaamuru Yakobo, ndugu yake Yohana, auawe kwa upanga. Alipoona jambo hilo limewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamkamata pia Petro. Hii ilitokea wakati wa Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Baada ya kumkamata alimtia gerezani, chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari, vyenye askari wanne kila kimoja. Herode alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka mbele ya watu baada ya Pasaka. Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii. Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza. Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro. Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.” Petro akatoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono. Wakapita lindo la kwanza na la pili, ndipo wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro. Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yoyote kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka makucha ya Herode Agripa na kutoka matazamio yote ya Wayahudi.” Mara Petro alipotambua hili alikwenda nyumbani kwa Maria, mama yake Yohana aliyeitwa pia Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekutana kwa maombi. Petro alipobisha hodi kwenye lango la nje, mtumishi wa kike jina lake Roda, akaja kumfungulia. Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi mno akarudi bila kufungua na kuwaeleza kwamba, “Petro yuko langoni!” Wakamwambia yule mtumishi wa kike, “Umerukwa na akili.” Alipozidi kusisitiza kuwa ni kweli, wakasema, “Lazima awe ni malaika wake.” Lakini Petro aliendelea kugonga langoni, nao walipofungua lango na kumwona Petro, walistaajabu sana.

Shirikisha
Soma Matendo 12