2 Timotheo 4:14-22
2 Timotheo 4:14-22 SRUV
Iskanda, mfua shaba, alionesha ubaya mwingi kwangu; Bwana atamlipa kulingana na matendo yake. Nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu. Katika utetezi wangu wa kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa kutoka kwa kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike katika ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina. Nisalimie Priska na Akila, na wale wa nyumbani mwa Onesiforo. Erasto alibaki Korintho. Trofimo nilimwacha huku Mileto, mgonjwa. Jitahidi uwezavyo kuja kabla ya majira ya baridi. Eubulo akusalimu, na Pude, na Lino, na Klaudia, na ndugu wote pia. Bwana na awe pamoja na roho yako. Neema na iwe pamoja nanyi.