2 Wafalme 14:8-22
2 Wafalme 14:8-22 SRUV
Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso. Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti. Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe? Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda. Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, dhiraa mia nne. Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria. Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa katika Samaria pamoja na wafalme wa Israeli; na Yeroboamu mwanawe akatawala mahali pake. Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli miaka kumi na mitano. Basi mambo yote ya Amazia yaliyosalia, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Wakafanya fitina juu yake katika Yerusalemu, naye akakimbia mpaka Lakishi, lakini wakatuma watu kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko. Wakamleta juu ya farasi; naye akazikwa huko Yerusalemu pamoja na babaze katika mji wa Daudi. Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa mwenye umri wa miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa baba yake Amazia. Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.