Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 14:8-22

2 Wafalme 14:8-22 NEN

Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tuonane uso kwa uso.” Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?” Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa 400. Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la BWANA na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria. Matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala pamoja na baba zake, akazikwa Samaria pamoja na wafalme wa Israeli, naye Yeroboamu mwanawe akawa mfalme baada yake. Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. Matukio mengine ya utawala wa Amazia, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Wakafanya shauri baya dhidi ya Amazia huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuulia huko. Akarudishwa kwa farasi na akazikwa huko Yerusalemu pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi. Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, na kumfanya mfalme mahali pa baba yake Amazia. Ndiye aliijenga tena Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.