Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 14:8-22

2 Wafalme 14:8-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli akisema, “Njoo tupambane.” Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia mfalme wa Israeli, akisema, “Siku moja mbaruti wa Lebanoni uliuambia mwerezi, wa huko Lebanoni pia, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu.’ Lakini mnyama wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mbaruti huo. Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?” Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda. Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yehoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi; halafu akauendea Yerusalemu na kuubomoa ukuta wake kutoka Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200. Alichukua dhahabu yote na fedha, hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu; pia alichukua mateka, kisha akarudi Samaria. Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Yehoashi alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria. Mwanae, Yeroboamu akatawala mahali pake. Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya mfalme Yehoashi wa Israeli kufariki. Matendo mengine yote ya Amazia yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Njama za kumwua Amazia zilifanywa Yerusalemu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi, lakini maadui walituma watu wa kumwua huko. Maiti yake ililetwa juu ya farasi na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika Yerusalemu katika mji wa Daudi. Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria akiwa na umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake. Azaria, baada ya kifo cha baba yake, aliujenga upya mji wa Elathi na kuurudisha kwa Yuda.

2 Wafalme 14:8-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso. Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti. Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe? Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda. Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, dhiraa mia nne. Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria. Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa katika Samaria pamoja na wafalme wa Israeli; na Yeroboamu mwanawe akatawala mahali pake. Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli miaka kumi na mitano. Basi mambo yote ya Amazia yaliyosalia, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Wakafanya fitina juu yake katika Yerusalemu, naye akakimbia mpaka Lakishi, lakini wakatuma watu kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko. Wakamleta juu ya farasi; naye akazikwa huko Yerusalemu pamoja na babaze katika mji wa Daudi. Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa mwenye umri wa miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa baba yake Amazia. Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.

2 Wafalme 14:8-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso. Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti. Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe? Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda. Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, mikono mia nne. Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria. Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa katika Samaria pamoja na wafalme wa Israeli; na Yeroboamu mwanawe akatawala mahali pake. Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli miaka kumi na mitano. Basi mambo yote ya Amazia yaliyosalia, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Wakafanya fitina juu yake katika Yerusalemu, naye akakimbia mpaka Lakishi, lakini wakatuma watu kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko. Wakamleta juu ya farasi; naye akazikwa huko Yerusalemu pamoja na babaze katika mji wa Daudi. Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa mwenye umri wa miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa baba yake Amazia. Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.

2 Wafalme 14:8-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tuonane uso kwa uso.” Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?” Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa 400. Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la BWANA na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria. Matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala pamoja na baba zake, akazikwa Samaria pamoja na wafalme wa Israeli, naye Yeroboamu mwanawe akawa mfalme baada yake. Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. Matukio mengine ya utawala wa Amazia, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Wakafanya shauri baya dhidi ya Amazia huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuulia huko. Akarudishwa kwa farasi na akazikwa huko Yerusalemu pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi. Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, na kumfanya mfalme mahali pa baba yake Amazia. Ndiye aliijenga tena Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.