2 Wakorintho 8:7-15
2 Wakorintho 8:7-15 SRUV
Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Nami katika neno hili natoa ushauri wangu; maana neno hili lawafaa ninyi mliotangulia, yapata mwaka, sio tu kutenda bali hata kutamani kutenda pia. Lakini sasa timizeni kule kutenda nako, ili kama vile mlivyokuwa tayari kutamani kutenda, vivyo hivyo mkawe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo. Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo. Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki; bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa.