2 Wakorintho 8:7-15
2 Wakorintho 8:7-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Nyinyi mna kila kitu: Imani, uwezo wa kusema, elimu; bidii yote ya kutenda mema, na upendo wenu kwetu. Hivyo, tunatazamia muwe wakarimu katika huduma hii ya upendo. Siwapi nyinyi amri, lakini nataka tu kuonesha jinsi wengine walivyo na bidii ya kusaidia ili nipate kujua jinsi upendo wenu ulivyo wa kweli. Maana, nyinyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: Yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake, awatajirishe. Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: Inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Nyinyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo. Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha. Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa; hadai zaidi. Nyinyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki. Kila mlicho nacho sasa cha ziada kiwasaidie wale wanaohitaji, ili nao wakati watakapokuwa na ziada, wawasaidie nyinyi katika mahitaji yenu, na hivyo kuwe na usawa. Kama Maandiko yasemavyo: “Aliyekusanya kwa wingi hakuwa na ziada, na yule aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”
2 Wakorintho 8:7-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Nami katika neno hili natoa ushauri wangu; maana neno hili lawafaa ninyi mliotangulia, yapata mwaka, sio tu kutenda bali hata kutamani kutenda pia. Lakini sasa timizeni kule kutenda nako, ili kama vile mlivyokuwa tayari kutamani kutenda, vivyo hivyo mkawe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo. Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo. Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki; bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa.
2 Wakorintho 8:7-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Nami katika neno hili natoa shauri langu; maana neno hili lawafaa ninyi mliotangulia, yapata mwaka, licha ya kutenda hata na kutaka pia. Lakini sasa timizeni kule kutenda nako, ili kama vile mlivyokuwa tayari kutaka, vivyo hivyo mkawe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo. Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo. Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki; bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa.
2 Wakorintho 8:7-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa. Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine. Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri. Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu juu ya jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo. Sasa ikamilisheni kazi hii kwa shauku kama mlivyoanza, jitoleeni kulingana na uwezo wenu. Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana. Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano. Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”