2 Wakorintho 8:7-15
2 Wakorintho 8:7-15 NEN
Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa. Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine. Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri. Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu juu ya jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo. Sasa ikamilisheni kazi hii kwa shauku kama mlivyoanza, jitoleeni kulingana na uwezo wenu. Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana. Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano. Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”