Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 25:23-44

1 Samweli 25:23-44 SRUV

Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifudifudi, akainama mpaka chini. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi sasa, bwana wangu, aishivyo BWANA, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa BWANA amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali. Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu. Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote. Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na BWANA, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya kombeo. Tena itakuwa, hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli; hili halitakuwa kikwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako. Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. Kwa kuwa ni kweli, aishivyo BWANA, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba usingalifanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mmoja wa kiume, kutakapopambazuka. Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimelikubali ombi lako. Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hadi kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, BWANA alimpiga huyo Nabali, hadi akafa. Naye Daudi aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, alisema, Na ahimidiwe BWANA ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumishi wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali BWANA amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe. Na hao watumishi wa Daudi walipomjia huyo Abigaili huko Karmeli, walimwambia, wakasema, Daudi ametutuma kwako ili tukutwae uwe mkewe. Naye akainuka na kujiinamisha kifudifudi mpaka chini, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumishi wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu. Abigaili akafanya haraka, akainuka, akapanda punda, pamoja na vijakazi watano wake waliofuatana naye, akawafuata hao wajumbe wa Daudi, akawa mkewe. Tena Daudi akamwoa Ahinoamu wa Yezreeli; wote wawili wakawa wake zake. Lakini Sauli alikuwa amemposa Mikali, binti yake aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti, mwana wa Laisha aliyekuwa mtu wa Galimu.