1 Samueli 25:23-44
1 Samueli 25:23-44 Biblia Habari Njema (BHN)
Abigaili alipomwona tu Daudi, akashuka mara moja kutoka juu ya punda wake, na kuinama mbele ya Daudi hadi uso wake ukagusa chini. Alijitupa miguuni pa Daudi na kumwambia, “Bwana wangu, hatia yote na iwe juu yangu tu. Nakuomba niongee nawe mimi mtumishi wako. Nakuomba usikilize maneno ya mtumishi wako. Usimfikirie Nabali ambaye ni mtu mbaya kwani lilivyo jina lake Nabali, ndivyo naye alivyo. Yeye anaitwa Nabali; na kweli yeye ni mtu mpumbavu. Bwana wangu, wale vijana wako ulipowatuma, mimi mtumishi wako sikuwaona. Sasa bwana wangu, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, na vile ulivyo hai, kwamba kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekuzuia usilipize kisasi kwa kumwaga damu na kujipatia lawama, waache adui zako na wale wote wanaokutakia mabaya wawe wapumbavu kama Nabali. Bwana wangu, nakuomba upokee zawadi hii niliyokuletea, na uwape vijana wanaokufuata. Nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako. Mwenyezi-Mungu atakupa jamaa imara kwa sababu, wewe bwana wangu, unapigana vita vya Mwenyezi-Mungu. Wakati wote wa maisha yako usipatikane na baa lolote. Kukitokea watu wakikufuatilia na kutaka kuyaangamiza maisha yako, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atayasalimisha maisha yako pamoja na walio hai. Lakini maisha ya adui zako atayatupilia mbali, kama vile mtu atupavyo jiwe kwa kombeo. Baada ya Mwenyezi-Mungu kukutendea mema yote aliyokuahidi, na kukuteua kuwa mtawala wa Israeli, wewe bwana wangu, hutakuwa na sababu ya kujuta wala kuhukumiwa na dhamiri kutokana na kumwaga damu bila sababu kwa kujilipiza kisasi. Lakini, bwana wangu, Mwenyezi-Mungu atakapokuwa amekutendea wema huo, nakuomba unikumbuke mimi mtumishi wako.” Daudi akamwambia Abigaili, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekutuma leo kukutana nami. Mtukuze Mwenyezi-Mungu aliyekupa busara kwa kunizuia kuwa na hatia ya umwagaji damu na kujilipiza kisasi mimi mwenyewe. Kwa hakika, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, amenizuia nisikudhuru. Usingefanya haraka kuja kukutana nami, kwa hakika, kesho asubuhi hakuna mwanamume yeyote wa Nabali angesalia.” Kisha, Daudi akapokea vitu vyote ambavyo Abigaili alikuwa amemletea, akamwambia Abigaili, “Rudi nyumbani kwako kwa amani. Tazama, mimi nimeyasikia uliyoyasema, na ombi lako nimelipokea.” Abigaili aliporudi nyumbani, alimkuta Nabali akifanya karamu kubwa nyumbani kwake kama ya kifalme. Nabali alikuwa ameburudika sana moyoni kwani alikuwa amelewa sana. Hivyo hakumwambia lolote mpaka asubuhi. Asubuhi, Abigaili alipoona mumewe divai imemtoka, alimweleza mambo yote, na papo hapo Nabali akapooza, akawa kama jiwe. Siku kumi baadaye, Mwenyezi-Mungu alimpiga Nabali akafa. Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, alisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amemlipiza kisasi Nabali kwa kunitukana, naye Mwenyezi-Mungu ameniepusha mimi mtumishi wake kutenda maovu. Mwenyezi-Mungu amempatiliza Nabali kwa uovu wake.” Kisha Daudi alituma watu ili wamposee Abigaili awe mke wake. Watumishi wa Daudi walipowasili kwa Abigaili huko Karmeli, wakamwambia, “Daudi ametutuma kukuchukua ili uwe mke wake.” Abigaili aliinuka, na kuinama mbele yao mpaka chini, akasema, “Mimi ni mtumishi tu; niko tayari kuosha miguu ya watumishi wa bwana wangu.” Abigaili alifanya haraka, akainuka na kupanda juu ya punda wake, akifuatana na watumishi wake wa kike watano, akaenda na watumishi wa Daudi; naye akawa mke wa Daudi. Tena Daudi alimwoa Ahinoamu kutoka Yezreeli. Hivyo hao wawili wakawa wake zake. Wakati huo, Shauli alikuwa amemwoza binti yake Mikali, ambaye alikuwa mke wa Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka mji wa Galimu.
1 Samueli 25:23-44 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifudifudi, akainama mpaka chini. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi sasa, bwana wangu, aishivyo BWANA, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa BWANA amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali. Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu. Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote. Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na BWANA, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya kombeo. Tena itakuwa, hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli; hili halitakuwa kikwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako. Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. Kwa kuwa ni kweli, aishivyo BWANA, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba usingalifanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mmoja wa kiume, kutakapopambazuka. Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimelikubali ombi lako. Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hadi kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, BWANA alimpiga huyo Nabali, hadi akafa. Naye Daudi aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, alisema, Na ahimidiwe BWANA ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumishi wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali BWANA amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe. Na hao watumishi wa Daudi walipomjia huyo Abigaili huko Karmeli, walimwambia, wakasema, Daudi ametutuma kwako ili tukutwae uwe mkewe. Naye akainuka na kujiinamisha kifudifudi mpaka chini, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumishi wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu. Abigaili akafanya haraka, akainuka, akapanda punda, pamoja na vijakazi watano wake waliofuatana naye, akawafuata hao wajumbe wa Daudi, akawa mkewe. Tena Daudi akamwoa Ahinoamu wa Yezreeli; wote wawili wakawa wake zake. Lakini Sauli alikuwa amemposa Mikali, binti yake aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti, mwana wa Laisha aliyekuwa mtu wa Galimu.
1 Samueli 25:23-44 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi sasa, bwana wangu, aishivyo BWANA, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa BWANA amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali. Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu. Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote. Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na BWANA, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya teo. Tena itakuwa, hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli; hili halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako. Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. Kwa kuwa ni kweli, aishivyo BWANA, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba hungefanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi. Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako. Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, BWANA alimpiga huyo Nabali, hata akafa. Naye aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, Daudi alisema, Na ahimidiwe BWANA ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumwa wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali BWANA amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe. Na hao watumishi wa Daudi walipomjia huyo Abigaili huko Karmeli, walimwambia, wakasema, Daudi ametutuma kwako ili tukutwae uwe mkewe. Naye akainuka na kujiinamisha kifulifuli mpaka nchi, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumwa wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu. Abigaili akafanya haraka, akainuka, akapanda punda, pamoja na vijakazi watano wake waliofuatana naye, akawafuata hao wajumbe wa Daudi, akawa mkewe. Tena Daudi akamwoa Ahinoamu wa Yezreeli; wakawa wote wawili wakeze. Walakini Sauli alikuwa amempa Palti, mwana wa Laishi, aliyekuwa mtu wa Galimu, Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi.
1 Samueli 25:23-44 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Abigaili alipomwona Daudi, akashuka haraka kwenye punda wake, akainama kifudifudi uso wake mpaka nchi mbele ya Daudi. Akamwangukia miguuni pake na kusema: “Bwana wangu, kosa hili na liwe juu yangu mwenyewe. Tafadhali mruhusu mtumishi wako aseme nawe. Sikia kile mtumishi wako atakachosema. Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake; jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye. Lakini kwangu mimi, mtumishi wako, sikuwaona hao watu waliotumwa na bwana wangu. “Basi sasa, kwa kuwa BWANA amekuzuia, wewe bwana wangu, kutokumwaga damu na kutolipiza kisasi kwa mikono yako mwenyewe, hakika kama BWANA aishivyo na kama uishivyo, maadui zako na wote wanaokusudia kumdhuru bwana wangu wawe kama Nabali. Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe. Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa BWANA kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya BWANA. Hata ingawa yuko mtu anayekufuatia kuuondoa uhai wako, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na BWANA Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako atavurumishwa kama vile jiwe kutoka kwenye kombeo. BWANA atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu yeye na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli, bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. BWANA atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.” Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli aliyekutuma kunilaki leo. Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu. La sivyo, hakika kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna hata mwanaume mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.” Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani kwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.” Abigaili alipokwenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote mpaka asubuhi yake. Basi asubuhi, Nabali alipokuwa amelevuka, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe. Baada ya siku kumi, BWANA akampiga Nabali, naye akafa. Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe BWANA, ambaye amenitetea shauri langu dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na BWANA ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.” Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake. Watumishi wa Daudi wakaenda mpaka Karmeli na kumwambia Abigaili, wakisema, “Daudi ametutuma kwako kukuchukua uwe mkewe.” Akainama chini uso wake mpaka ardhini, akasema, “Mjakazi wako yuko hapa, tayari kuwatumikia na kuwanawisha miguu watumishi wa bwana wangu.” Abigaili akainuka kwa haraka, akapanda punda wake, akihudumiwa na wajakazi wake watano, akaenda pamoja na wajumbe wa Daudi, naye akawa mkewe. Pia Daudi alikuwa amemwoa Ahinoamu wa Yezreeli, wote wawili wakawa wake zake. Lakini Sauli alikuwa amemwoza Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka Galimu.