1 Samweli 25:23-44
1 Samweli 25:23-44 NEN
Abigaili alipomwona Daudi, akashuka haraka kwenye punda wake, akainama kifudifudi uso wake mpaka nchi mbele ya Daudi. Akamwangukia miguuni pake na kusema: “Bwana wangu, kosa hili na liwe juu yangu mwenyewe. Tafadhali mruhusu mtumishi wako aseme nawe. Sikia kile mtumishi wako atakachosema. Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake; jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye. Lakini kwangu mimi, mtumishi wako, sikuwaona hao watu waliotumwa na bwana wangu. “Basi sasa, kwa kuwa BWANA amekuzuia, wewe bwana wangu, kutokumwaga damu na kutolipiza kisasi kwa mikono yako mwenyewe, hakika kama BWANA aishivyo na kama uishivyo, maadui zako na wote wanaokusudia kumdhuru bwana wangu wawe kama Nabali. Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe. Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa BWANA kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya BWANA. Hata ingawa yuko mtu anayekufuatia kuuondoa uhai wako, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na BWANA Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako atavurumishwa kama vile jiwe kutoka kwenye kombeo. BWANA atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu yeye na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli, bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. BWANA atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.” Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli aliyekutuma kunilaki leo. Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu. La sivyo, hakika kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna hata mwanaume mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.” Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani kwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.” Abigaili alipokwenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote mpaka asubuhi yake. Basi asubuhi, Nabali alipokuwa amelevuka, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe. Baada ya siku kumi, BWANA akampiga Nabali, naye akafa. Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe BWANA, ambaye amenitetea shauri langu dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na BWANA ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.” Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake. Watumishi wa Daudi wakaenda mpaka Karmeli na kumwambia Abigaili, wakisema, “Daudi ametutuma kwako kukuchukua uwe mkewe.” Akainama chini uso wake mpaka ardhini, akasema, “Mjakazi wako yuko hapa, tayari kuwatumikia na kuwanawisha miguu watumishi wa bwana wangu.” Abigaili akainuka kwa haraka, akapanda punda wake, akihudumiwa na wajakazi wake watano, akaenda pamoja na wajumbe wa Daudi, naye akawa mkewe. Pia Daudi alikuwa amemwoa Ahinoamu wa Yezreeli, wote wawili wakawa wake zake. Lakini Sauli alikuwa amemwoza Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka Galimu.