Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 14:1-23

1 Samweli 14:1-23 SRUV

Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na tuvuke twende kwa Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Lakini hakumwarifu babaye. Naye Sauli alikuwa akikaa katika Viunga vya Gibea, chini ya mkomamanga uliokuwa kwenye uwanja huko Migroni; na hao watu waliokuwa pamoja naye walikuwa watu mia sita; pamoja na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, aliyevaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. Na katikati ya mapito, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na kilima cha mwamba upande huu, na kilima cha mwamba upande huu; kimoja kiliitwa Bosesi, na cha pili Sene. Hicho kilima kimoja kimesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hicho cha pili upande wa kusini, mbele ya Geba. Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na twende tukavuke ngomeni mwa hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kama ni kwa wengi au kama ni kwa wachache. Naye huyo mbebaji silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako. Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutavuka kwa watu hawa, na kujidhihirisha kwao. Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hadi sisi tuwafikie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwaendee. Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, njoni; hapo ndipo tutakapoenda; kwa maana BWANA amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu. Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania wanatoka katika mashimo walimojificha! Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mbebaji silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa BWANA amewatia mikononi mwa Israeli. Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mbebaji silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mbemba silaha zake akawaua akiwa nyuma yake. Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulikuwa kama watu ishirini, katika eneo la kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima. Kukawa na tetemeko katika kambi, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno. Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huku na huko. Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yule aliyembebea silaha zake hawakuwapo. Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu, wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli. Ikawa Sauli alipokuwa akisema na kuhani, hayo makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudi, usiendee sanduku la Mungu. Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa. Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka kambini toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani. Hivyo BWANA akawaokoa Israeli siku ile; na vita ilienea mpaka kupita Beth-aveni, na watu wote waliokuwa pamoja na Sauli walikuwa kama wanaume elfu kumi. Vita ikanenea katika nchi yenye milima milima ya Efraimu.