1 Samueli 14:1-23
1 Samueli 14:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Yonathani mwana wa mfalme Shauli alimwambia kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende ngambo kwenye ngome ya Wafilisti.” Lakini Yonathani hakumwambia baba yake. Shauli alikuwa amepiga kambi chini ya mkomamanga huko Migroni, nje ya mji wa Gibea, akiwa pamoja na watu wapatao 600. Ahiya, mwana wa Ahitubu ndugu yake Ikabodi mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi-Mungu mjini Shilo, alikuwa ndiye aliyevaa kizibao cha kuhani. Watu hawakujua kwamba Yonathani amekwisha ondoka. Kwenye kipito ambako Yonathani alipaswa apitie ili afike kwenye ngome ya Wafilisti, kulikuwa na miamba miwili iliyochongoka, upande huu na upande mwingine. Mwamba mmoja uliitwa Bosesi na mwingine uliitwa Sene. Mwamba mmoja ulikuwa kaskazini mwa mji wa Mikmashi na mwingine ulikuwa kusini mkabala na mji wa Gibea. Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende upande wa pili kwenye ile ngome ya hawa watu wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi-Mungu akatusaidia, maana Mwenyezi-Mungu haokoi kwa kutegemea wingi au uchache wa watu.” Yule kijana aliyembebea silaha akamwambia, “Fanya chochote unachotaka kufanya, mimi niko pamoja nawe kwani wazo lako ndilo wazo langu.” Yonathani akamwambia, “Tutavuka kuwaendea wale watu ili wapate kutuona. Kama wakituambia tuwangoje, hadi waje hapa tulipo basi, tutasimama papa hapa na wala hatutawaendea. Lakini wakisema sisi tuwaendee, basi tutawaendea kwani hiyo itakuwa ni ishara kuwa Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwetu.” Basi, wakajitokeza ili Wafilisti wawaone. Wafilisti walipowaona wakasema, “Angalieni wale Waebrania wanatoka kwenye mashimo walimokuwa wamejificha.” Wafilisti waliokuwa kwenye ngome wakamwita Yonathani na kijana aliyembebea silaha, “Njoni huku kwetu, nasi tutawaonesha kitu.” Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Nifuate; Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwa Israeli.” Basi, Yonathani akapanda kwa miguu na mikono, na yule kijana akamfuata. Yonathani aliwashambulia Wafilisti akiwaangusha chini huku yule kijana alifuata nyuma akiwaua. Katika mashambulizi hayo ya kwanza Yonathani, akiwa pamoja na kijana wake aliyembebea silaha, aliwaua watu kama ishirini katika eneo la nchi lipatalo nusu eka. Katika nchi nzima ya Wafilisti, wote walianza kufadhaika, wanajeshi kambini, watu mashambani, kwenye ngome, hata na washambuliaji walitetemeka; nchi ilitetemeka, na kulikuwa na woga mkubwa. Wapelelezi wa Shauli huko Gibea katika nchi ya Benyamini waliwaona watu wengi wakikimbia huku na huko. Shauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, “Hebu jihesabuni ili kujua ni akina nani waliotutoroka.” Walipojihesabu, waligundua kuwa Yonathani na kijana aliyembebea silaha walikuwa hawapo. Shauli akamwambia kuhani Ahiya, “Lilete hapa sanduku la Mungu.” (Wakati huo sanduku la agano la Mungu lilikuwa pamoja na Waisraeli.) Shauli alipokuwa anaongea bado na kuhani, ghasia kambini kwa Wafilisti ziliongezeka zaidi na zaidi. Kwa hiyo Shauli akamwambia kuhani, “Acha; usililete tena sanduku la agano.” Hivyo, Shauli na watu wake wakajipanga na kuingia vitani dhidi ya Wafilisti. Lakini Wafilisti walianza kushambuliana wenyewe kwa wenyewe kwa mvurugiko mkubwa. Waebrania waliokuwa upande wa Wafilisti, na waliokwenda nao huko kambini, wakageuka na kujiunga na Waisraeli waliokuwa pamoja na Shauli na Yonathani. Hata Waisraeli wengine waliokuwa wamejificha kwenye nchi ya milima ya Efraimu, waliposikia kuwa Wafilisti walikuwa wanakimbia, nao pia wakawafuatia na kuwapiga. Hivyo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi.
1 Samueli 14:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na tuvuke twende kwa Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Lakini hakumwarifu babaye. Naye Sauli alikuwa akikaa katika Viunga vya Gibea, chini ya mkomamanga uliokuwa kwenye uwanja huko Migroni; na hao watu waliokuwa pamoja naye walikuwa watu mia sita; pamoja na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, aliyevaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. Na katikati ya mapito, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na kilima cha mwamba upande huu, na kilima cha mwamba upande huu; kimoja kiliitwa Bosesi, na cha pili Sene. Hicho kilima kimoja kimesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hicho cha pili upande wa kusini, mbele ya Geba. Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na twende tukavuke ngomeni mwa hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kama ni kwa wengi au kama ni kwa wachache. Naye huyo mbebaji silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako. Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutavuka kwa watu hawa, na kujidhihirisha kwao. Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hadi sisi tuwafikie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwaendee. Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, njoni; hapo ndipo tutakapoenda; kwa maana BWANA amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu. Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania wanatoka katika mashimo walimojificha! Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mbebaji silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa BWANA amewatia mikononi mwa Israeli. Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mbebaji silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mbemba silaha zake akawaua akiwa nyuma yake. Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulikuwa kama watu ishirini, katika eneo la kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima. Kukawa na tetemeko katika kambi, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno. Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huku na huko. Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yule aliyembebea silaha zake hawakuwapo. Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu, wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli. Ikawa Sauli alipokuwa akisema na kuhani, hayo makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudi, usiendee sanduku la Mungu. Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa. Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka kambini toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani. Hivyo BWANA akawaokoa Israeli siku ile; na vita ilienea mpaka kupita Beth-aveni, na watu wote waliokuwa pamoja na Sauli walikuwa kama wanaume elfu kumi. Vita ikanenea katika nchi yenye milima milima ya Efraimu.
1 Samueli 14:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na tuwavukie Wafilisti ngomeni, pale ng’ambo ya pili. Walakini hakumwarifu babaye. Naye Sauli alikuwa akikaa katika upande wa mwisho wa Giba, chini ya mkomamanga ulioko kwenye uga; na hao watu waliokuwa pamoja naye walipata watu mia sita; na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, mwenye kuvaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. Na katikati ya mianya, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikilia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na genge la jabali upande huu, na genge la jabali upande huu; jina la moja liliitwa Bosesi, na jina la pili Sene. Hilo genge moja limesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hilo la pili upande wa kusini, mbele ya Geba. Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache. Naye huyo mchukua silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako. Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutawavukia watu hawa, na kujidhihirisha kwao. Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hata sisi tuwafikilie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwapandie. Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, tupandieni sisi; hapo ndipo tutakapopanda; kwa maana BWANA amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu. Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania watoka katika mashimo walimojificha! Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mchukua silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonyesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa BWANA amewatia mikononi mwa Israeli. Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mchukua silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mchukua silaha zake akawaua nyuma yake. Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulipata kama watu ishirini, katika nafasi kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima. Kukawa na tetemeko katika marago, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji wa nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno. Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huko na huko. Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yeye aliyechukua silaha zake hawapo. Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli. Ikawa Sauli alipokuwa katika kusema na kuhani, hayo makelele katika marago ya Wafilisti yakaendelea na kuzidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudisha mkono wako. Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa. Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka maragoni toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani. Hivyo BWANA akawaokoa Israeli siku ile; na vita vikapita mbele karibu na Beth-aveni. Wakati huo mbele ya wana wa Israeli.
1 Samueli 14:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake. Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu kama 600, miongoni mwao alikuwepo Ahiya, ambaye alikuwa amevaa kisibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka. Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwepo na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene. Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba. Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda BWANA atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia BWANA kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.” Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.” Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone. Kama wakituambia, ‘Subirini hapo mpaka tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao. Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba BWANA amewatia mikononi mwetu.” Basi wote wawili wakajionyesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.” Watu wa kwenye doria wakawapigia kelele Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu nasi tutawakomesha.” Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; BWANA amewatia mikononi mwa Israeli.” Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake. Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka. Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo nchi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu. Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote. Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka katikati yetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo. Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.) Wakati Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.” Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake. Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii. Hivyo BWANA akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni.