1 Samweli 14:1-23
1 Samweli 14:1-23 NEN
Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake. Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu kama 600, miongoni mwao alikuwepo Ahiya, ambaye alikuwa amevaa kisibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka. Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwepo na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene. Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba. Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda BWANA atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia BWANA kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.” Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.” Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone. Kama wakituambia, ‘Subirini hapo mpaka tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao. Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba BWANA amewatia mikononi mwetu.” Basi wote wawili wakajionyesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.” Watu wa kwenye doria wakawapigia kelele Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu nasi tutawakomesha.” Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; BWANA amewatia mikononi mwa Israeli.” Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake. Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka. Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo nchi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu. Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote. Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka katikati yetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo. Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.) Wakati Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.” Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake. Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii. Hivyo BWANA akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni.