Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 11:14-25

1 Wafalme 11:14-25 SRUV

Ndipo BWANA akamwinulia Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; aliyekuwa wa wazawa wake mfalme wa Edomu. Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu, (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hadi alipompoteza kila mwanamume wa Edomu); yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi angali ni mtoto mdogo. Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akaamuru apewe vyakula, akampa mashamba. Hadadi akapendeza sana machoni pa Farao, hata akamwoza dada ya mkewe, dada ya Tapanesi aliyekuwa malkia. Naye huyo dada ya Tapanesi akamzalia Genubathi mwanawe, ambaye Tapanesi alimlea nyumbani mwa Farao; naye Genubathi akawako nyumbani mwa Farao pamoja na wana wa Farao. Naye Hadadi aliposikia huko Misri ya kuwa Daudi amelala na babaze, na Yoabu, jemadari wa jeshi, amekufa, Hadadi akamwambia Farao, Unipe ruhusa, niende mpaka nchi yangu. Farao akamwambia, Umekosa nini kwangu, hata, tazama, unatafuta kuirudia nchi yako? Akajibu, Hakuna, lakini unipe ruhusa tu. Tena, Mungu akamwinulia adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba, naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski. Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.