1 Wafalme 11:14-25
1 Wafalme 11:14-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo BWANA akamwinulia Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; aliyekuwa wa wazawa wake mfalme wa Edomu. Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu, (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hadi alipompoteza kila mwanamume wa Edomu); yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi angali ni mtoto mdogo. Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akaamuru apewe vyakula, akampa mashamba. Hadadi akapendeza sana machoni pa Farao, hata akamwoza dada ya mkewe, dada ya Tapanesi aliyekuwa malkia. Naye huyo dada ya Tapanesi akamzalia Genubathi mwanawe, ambaye Tapanesi alimlea nyumbani mwa Farao; naye Genubathi akawako nyumbani mwa Farao pamoja na wana wa Farao. Naye Hadadi aliposikia huko Misri ya kuwa Daudi amelala na babaze, na Yoabu, jemadari wa jeshi, amekufa, Hadadi akamwambia Farao, Unipe ruhusa, niende mpaka nchi yangu. Farao akamwambia, Umekosa nini kwangu, hata, tazama, unatafuta kuirudia nchi yako? Akajibu, Hakuna, lakini unipe ruhusa tu. Tena, Mungu akamwinulia adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba, naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski. Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.
1 Wafalme 11:14-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo BWANA akamwondokeshea Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; yeye alikuwa wa wazao wake mfalme wa Edomu. Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu, (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hata alipompoteza kila mwanamume wa Edomu); yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi akali ni mtoto mdogo. Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akamwamria vyakula, akampa mashamba. Hadadi akapendeza sana machoni pa Farao, hata akamwoza umbu la mkewe, umbu la Tapenesi aliyekuwa malkia. Naye huyo umbu la Tapenesi akamzalia Genubathi mwanawe, ambaye Tapenesi alimlea nyumbani mwa Farao; naye Genubathi akawako nyumbani mwa Farao pamoja na wana wa Farao. Naye Hadadi aliposikia huko Misri ya kuwa Daudi amelala na babaze, na Yoabu, jemadari wa jeshi, amekufa, Hadadi akamwambia Farao, Unipe ruhusa, niende mpaka nchi yangu. Farao akamwambia, Umekosa nini kwangu, hata, tazama, unatafuta kuirudia nchi yako? Akajibu, Hakuna, lakini unipe ruhusa tu. Tena, Mungu akamwondokeshea adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba, naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski. Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.
1 Wafalme 11:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo Mwenyezi-Mungu akamfanya Hadadi aliyekuwa wa ukoo wa mfalme wa Edomu, kuwa adui ya Solomoni. Wakati Daudi alipowaangamiza Waedomu Yoabu, mkuu wa jeshi la Daudi, alikwenda huko kuwazika waliouawa. Yoabu aliwaua wanaume wote wa Edomu. (Yoabu alikaa huko na wanajeshi wake kwa muda wa miezi sita, apate kuwaangamiza kabisa wanaume wote wa Edomu.) Lakini Hadadi ambaye wakati huo alikuwa kijana alitorokea Misri pamoja na Waedomu kadhaa, watumishi wa baba yake. Hadadi na wenzake walisafiri kutoka Midiani, wakawachukua watu wengine huko Parani, wakaenda nao mpaka Misri, kwa Farao mfalme wa nchi hiyo. Farao akampatia Hadadi nyumba, akaamuru awe akipewa chakula, akampa na ardhi. Farao alipendezwa sana na Hadadi. Hivyo Farao akamruhusu shemeji yake, mdogo wa malkia Tapenesi, aolewe na Hadadi. Huyo dada wa Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi. Genubathi alilelewa na Tapenesi katika nyumba ya Farao, pamoja na wana wa mfalme. Lakini Hadadi aliposikia huko Misri kwamba Daudi na Yoabu mkuu wa jeshi, walikuwa wamefariki, alimwambia Farao, “Uniruhusu niondoke nirudi nchini kwangu.” Lakini Farao akamwuliza, “Nimekunyima nini hata uamue sasa kurudi nchini kwako?” Naye Hadadi akamsihi akisema, “Uniache tu niende.” Vilevile, Mungu alimfanya Rezoni mwana wa Eliada, awe adui ya Solomoni. Rezoni alikuwa amemtoroka bwana wake, mfalme Hadadezeri wa Soba. Baada ya Daudi kufanya mauaji huko Soba, Rezoni alikusanya watu na kuunda genge la maharamia, naye mwenyewe akawa kiongozi wao. Basi, wakaenda Damasko, wakakaa huko na kumfanya Rezoni mfalme wa Damasko. Rezoni alikuwa adui wa Israeli siku zote za utawala wa Solomoni, akamsumbua sana Solomoni kama naye Hadadi alivyomsumbua. Basi, Rezoni aliidharau Israeli, naye alitawala nchi ya Aramu.
1 Wafalme 11:14-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha BWANA akamwinua adui dhidi ya Solomoni, Hadadi, Mwedomu, kutoka ukoo wa ufalme wa Edomu. Huko nyuma wakati Daudi alipokuwa akipigana na Edomu, Yoabu jemadari wa jeshi, aliyekuwa amekwenda kuzika waliouawa, alikuwa amewaua wanaume wote waliokuwako Edomu. Yoabu na Waisraeli wote walikaa huko kwa miezi sita, mpaka walipomaliza kuwaangamiza wanaume wote huko Edomu. Lakini Hadadi, akiwa bado mvulana mdogo, alikimbilia Misri akiwa na baadhi ya maafisa wa Kiedomu waliokuwa wakimhudumia baba yake. Wakaondoka Midiani wakaenda Parani. Basi wakichukua pamoja nao wanaume kutoka Parani, wakaenda Misri, kwa Farao mfalme wa Misri, ambaye alimpa Hadadi nyumba, ardhi na akampatia chakula. Farao akapendezwa sana na Hadadi hata akampa ndugu wa mkewe mwenyewe, Malkia Tapenesi, ili aolewe na Hadadi. Huyo ndugu wa Tapenesi akamzalia mwana aliyeitwa Genubathi, ambaye alilelewa na Tapenesi katika jumba la kifalme. Huko Genubathi aliishi pamoja na watoto wa Farao mwenyewe. Alipokuwa huko Misri, Hadadi alisikia kwamba Daudi amepumzika na baba zake na ya kwamba pia Yoabu aliyekuwa jemadari wa jeshi amekufa. Ndipo Hadadi akamwambia Farao, “Niruhusu niende ili niweze kurudi katika nchi yangu.” Farao akauliza, “Umekosa nini hapa, kwamba unataka kurudi katika nchi yako?” Hadadi akajibu, “Hakuna, lakini niruhusu niende!” Mungu akamwinua adui mwingine dhidi ya Solomoni, Rezoni mwana wa Eliada, ambaye alikuwa amemkimbia bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba. Akawakusanya watu, naye akawa kiongozi wa kundi la waasi, wakati Daudi alipoangamiza majeshi ya Soba; waasi walikwenda Dameski, mahali walipokaa na kumiliki. Rezoni alikuwa adui wa Israeli kwa muda wote alioishi Solomoni, ukiongezea matatizo yaliyosababishwa na Hadadi. Kwa hiyo Rezoni akatawala katika Aramu na alikuwa mkatili kwa Israeli.