Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 11:14-25

1 Wafalme 11:14-25 NENO

Kisha Mwenyezi Mungu akamwinua adui dhidi ya Sulemani, Hadadi, Mwedomu, kutoka ukoo wa ufalme wa Edomu. Hapo awali Daudi alipokuwa akipigana na Edomu, Yoabu jemadari wa jeshi, aliyekuwa ameenda kuzika waliouawa, alikuwa amewaua wanaume wote katika Edomu. Yoabu na Waisraeli wote walikaa huko kwa miezi sita, hadi walipomaliza kuwaangamiza wanaume wote huko Edomu. Lakini Hadadi, akiwa bado mvulana mdogo, alikimbilia Misri akiwa na baadhi ya maafisa wa Edomu waliokuwa wamemhudumia baba yake. Wakatoka Midiani wakaenda hadi Parani. Wakawachukua watu kutoka Parani, wakaenda nao Misri kwa Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimpa Hadadi nyumba na shamba, na pia chakula. Farao akapendezwa sana na Hadadi, hata akampa dada ya mkewe, Malkia Tapenesi, awe mke wake. Huyo dada yake Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi, ambaye alilelewa na Tapenesi katika jumba la kifalme. Huko, Genubathi akaishi pamoja na watoto wa Farao. Alipokuwa huko Misri, Hadadi alisikia kwamba Daudi amelala na baba zake, na kwamba Yoabu aliyekuwa jemadari wa jeshi pia amekufa. Ndipo Hadadi akamwambia Farao, “Niruhusu niende ili nirudi nchi yangu.” Farao akauliza, “Umekosa nini hapa, kwamba unataka kurudi katika nchi yako?” Hadadi akajibu, “Hakuna, lakini niruhusu niende!” Mungu akamwinua adui mwingine dhidi ya Sulemani, Rezoni mwana wa Eliada, aliyekuwa amemkimbia bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba. Akawakusanya watu, naye akawa kiongozi wa kundi la waasi, wakati Daudi alipoangamiza majeshi ya Soba; waasi walienda Dameski, mahali walipokaa na kumiliki. Rezoni alikuwa adui wa Israeli kwa muda wote alioishi Sulemani, kuongezea matatizo yaliyosababishwa na Hadadi. Kwa hiyo Rezoni akatawala katika Aramu na akawa mkatili kwa Israeli.