1 Mambo ya Nyakati 26:1-32
1 Mambo ya Nyakati 26:1-32 SRUV
Kwa zamu zao mabawabu; wa Wakora; Meshelemia mwana wa Kore, wa wana wa Ebiasafu. Naye Meshelemia alikuwa na wana; Zekaria mzaliwa wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne; Elamu wa tano, Yohana wa sita, Elioenai wa saba. Naye Obed-edomu alikuwa na wana; Shemaya mzaliwa wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, na Sakari wa nne, na Nethaneli wa tano; Amieli wa sita, Isakari wa saba, Peulethai wa nane; kwa jinsi Mungu alivyombariki. Naye mwanawe Shemaya akazaliwa wana, walioongoza ukoo wa baba yao; kwa kuwa walikuwa wanaume mashujaa. Wana wa Shemaya; Othni, na Refaeli, na Obedi, na Elzabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu, na Semakia. Hao wote walikuwa wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, watu hodari wawezao huo utumishi; watu wa Obed-edomu sitini na wawili. Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze, watu mashujaa, kumi na wanane. Hosa naye, wa wana wa Merari, alikuwa na wana; Shimri mkuu wao; (kwani ajapokuwa yeye si mzaliwa wa kwanza, babaye alimweka mkuu); Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu, Zekaria wa nne; wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa watu kumi na watatu. Katika hao zilikuwa zamu za mabawabu, yaani, katika hao wakuu, wenye huduma kama ndugu zao, wa kutumika katika nyumba ya BWANA. Nao wakapigiwa kura kwa ajili ya kila lango, wadogo na wakubwa kwa pamoja, kwa kufuata koo za baba zao. Kura ya lango la mashariki ikamwangukia Meshelemia. Ndipo wakamtupia kura Zekaria mwanawe, mshauri mwenye busara; na kura yake ikamtokea ya kaskazini. Ya Obed-edomu ya kusini; na ya wanawe nyumba ya akiba. Ya Shupimu na Hosa upande wa magharibi, langoni pa Shalekethi, hapo penye daraja ya kupandia, ulinzi ulifanywa kwa zamu. Upande wa mashariki walikuwapo Walawi sita, kaskazini wanne kila siku, kusini wanne kila siku, na wa nyumba ya akiba wawili wawili. Penye Parbari upande wa magharibi, walikuwapo wanne darajani, na wawili huko Parbari. Hizo ndizo zamu za mabawabu; wa wana wa Wakora, na wa wana wa Merari. Na katika Walawi; Ahia mtunzaji wa hazina ya nyumba ya Mungu, pamoja na hazina ya vitu vilivyowekwa wakfu. Wana wa Ladani; wana wa Wagershoni waliokuwa wa Ladani; wakuu wa koo za mababa waliokuwa wa Ladani, Mgershoni; Yehieli. Wana wa Yehieli; Zethamu, na Yoeli nduguye, walikuwa watunzaji wa hazina ya nyumba ya BWANA. Wa Waamrami wa Waishari, wa Wahebroni, wa Wauzieli; na Shebueli, mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, alikuwa mtunzaji wa hazina zote. Na nduguze; wa Eliezeri, Rehabia mwanawe, na Ishia mwanawe, na Yoramu mwanawe, na Zikri mwanawe, na Shelomothi mwanawe. Huyo Shelomothi na ndugu zake walikuwa wasimamizi wa hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyoviweka wakfu mfalme Daudi, na hao wakuu wa koo za mababa, na maofisa wa maelfu na wa mamia, na makamanda wa jeshi. Katika nyara zilizopatikana vitani, waliweka wakfu sehemu, ili kuitengeneza nyumba ya BWANA. Na vyote alivyoviweka wakfu Samweli mwonaji, na Sauli mwana wa Kishi, na Abneri mwana wa Neri, na Yoabu mwana wa Seruya; na mtu yeyote aliyekiweka wakfu kitu chochote, kilikuwa chini ya mkono wa Shelomothi na nduguze. Katika Waishari, Kenania na wanawe walikuwa kwa ajili ya kazi ya nje juu ya Israeli, kuwa maofisa na waamuzi. Katika Wahebroni, Hashabia na nduguze, mashujaa, elfu moja na mia saba, walikuwa na usimamizi juu ya Israeli ng'ambo ya Yordani upande wa magharibi; kwa ajili ya kazi zote za BWANA, na kwa utumishi wa mfalme. Katika Wahebroni Yeria alikuwa mkuu, yaani, wa hao Wahebroni kwa kufuata vizazi vyao kwa koo za mababa. Katika mwaka arubaini wa kutawala kwake Daudi wakatafutwa, wakaonekana huko Yazeri ya Gileadi miongoni mwao wanaume mashujaa. Na nduguze, mashujaa, walikuwa elfu mbili na mia saba, wakuu wa koo za mababa, ambao mfalme Daudi aliwaweka wawe wasimamizi juu ya Wareubeni, na Wagadi, na nusu kabila la Wamanase, kwa ajili ya kila neno lililomhusu Mungu, na kwa mambo ya mfalme.