Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 26:1-32

1 Mambo ya Nyakati 26:1-32 Biblia Habari Njema (BHN)

Haya ndiyo makundi ya Walawi waliofanya kazi za ubawabu. Kutoka katika ukoo wa Kora, alikuwa Meshelemia mwana wa Kore wa jamaa ya Asafu. Yeye alikuwa na wana saba: Zekaria mzaliwa wake wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne, Elamu wa tano, Yohanani wa sita na Eliehoenai wa saba. Pia kulikuwa na Obed-edomu, ambaye Mungu alimbariki kwa kumpa wana wanane: Shemaya mzaliwa wake wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, Sakari wa nne, Nethaneli wa tano, Amieli wa sita, Isakari wa saba na Peulethai wa nane. Naye mwanawe Shemaya alipata wana waliokuwa na mamlaka juu ya jamaa ya baba yao, kwa sababu walikuwa wanaume wenye uwezo mkubwa. Shemaya, mzaliwa wa kwanza wa Obed-edomu, alikuwa na wana sita: Othni, Refaeli, Obedi, Elizabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu na Semakia. Hao wote wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, walikuwa watu hodari wawezao huo utumishi. Wazawa wote wa Obed-edomu walikuwa sitini na wawili. Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze; watu wenye uwezo kumi na wanne. Hosa mmojawapo wa wana wa Merari alikuwa na wana wanne: Shimri (aliyefanywa kiongozi na baba yake hata ingawa hakuwa mzaliwa wa kwanza), Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu na Zekaria wa nne. Wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa kumi na watatu. Mabawabu hao waligawanyika katika makundi kulingana na jamaa zao, nao pia walipangiwa kazi kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu kama wale Walawi wengine. Kila jamaa, bila kujali wingi, ilipiga kura kuchagua lango watakalosimamia. Kura ya kuchagua wa kulinda lango la mashariki ilimwangukia Shelemia. Walipiga kura pia kwa ajili ya mwanawe Zekaria, aliyekuwa mshauri mwenye busara, ikamwangukia kura ya lango la kaskazini. Obed-edomu aliangukiwa na kura ya lango la kusini, na ya wanawe, ghala. Shupimu na Hosa waliangukiwa na kura ya kulinda lango la magharibi kwenye lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu. Ulinzi ulifanywa kwa zamu. Kila siku upande wa mashariki kulikuwa na mabawabu sita, kaskazini wanne, na kusini wanne, pia kwenye ghala kuliwekwa mabawabu wawiliwawili. Kwenye banda zuri lililokuwa upande wa magharibi, kulikuwa na mabawabu wanne barabarani, na wawili kwenye banda lenyewe. Haya ndiyo makundi ya mabawabu miongoni mwa ukoo wa Kora na wazawa wa Merari waliofanya kazi ya ubawabu. Miongoni mwa Walawi, Ahiya alihusika na uangalizi wa hazina ya nyumba ya Mungu, na hazina ya vitu vilivyowekwa wakfu. Ladani, mmoja wa ukoo wa Gershoni, alikuwa babu wa baadhi ya jamaa, miongoni mwao ikiwamo jamaa ya mwanawe Yehieli. Wana wengine wawili wa Ladani, Zethamu na Yoeli, walikuwa watunzaji wa hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Pia kazi ziligawanywa kwa watu wa koo za Wasiria, Waishari, Wahebroni na Wauzieli. Shebueli, mwana wa Gershoni, mwana wa Mose, alikuwa ofisa mkuu wa hazina hizo. Na ndugu yake, alikuwa Eliezeri, aliyekuwa baba yake Rehabia, aliyemzaa Yeshaya, aliyemzaa Yoramu, aliyemzaa Zikri, aliyemzaa Shelomithi. Shelomithi na ndugu zake, ndio waliokuwa waangalizi wa hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu na mfalme Daudi, na viongozi wa jamaa, maofisa wa maelfu na mamia na majemadari wa jeshi. Waliweka wakfu sehemu ya nyara walizoteka vitani kwa ajili ya matengenezo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Pia, vitu vyote vilivyowekwa wakfu na Samueli, mwonaji, na Shauli mwana wa Kishi, na Abneri, na Yoabu mwana wa Seruya, vilikuwa chini ya uangalizi wa Shelomithi na nduguze. Miongoni mwa Waishari, Kenania na wanawe walipewa kazi za utawala kama maofisa na waamuzi, kwa ajili ya Waisraeli. Miongoni mwa Wahebroni, Hashabia na nduguze 1,700, wote watu mashujaa walipewa wajibu wa kusimamia sehemu za Israeli zilizokuwa upande wa magharibi wa mto Yordani. Walisimamia kazi yote ya Mwenyezi-Mungu na kazi za mfalme Daudi. Miongoni mwa Wahebroni, Yeria alikuwa kiongozi wa koo na jamaa zote, na katika mwaka wa arubaini wa utawala wa mfalme Daudi, uchunguzi ulifanywa, na wanaume wenye uwezo mkubwa walipatikana huko Yezeri katika Gileadi. Mfalme Daudi alimteua Yeriya na ndugu zake 2,700, mashujaa na viongozi wa koo, kusimamia mambo yote yaliyohusu Mungu na mfalme Daudi katika sehemu za Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, zilizokuwa mashariki ya mto Yordani.

1 Mambo ya Nyakati 26:1-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kwa zamu zao mabawabu; wa Wakora; Meshelemia mwana wa Kore, wa wana wa Ebiasafu. Naye Meshelemia alikuwa na wana; Zekaria mzaliwa wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne; Elamu wa tano, Yohana wa sita, Elioenai wa saba. Naye Obed-edomu alikuwa na wana; Shemaya mzaliwa wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, na Sakari wa nne, na Nethaneli wa tano; Amieli wa sita, Isakari wa saba, Peulethai wa nane; kwa jinsi Mungu alivyombariki. Naye mwanawe Shemaya akazaliwa wana, walioongoza ukoo wa baba yao; kwa kuwa walikuwa wanaume mashujaa. Wana wa Shemaya; Othni, na Refaeli, na Obedi, na Elzabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu, na Semakia. Hao wote walikuwa wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, watu hodari wawezao huo utumishi; watu wa Obed-edomu sitini na wawili. Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze, watu mashujaa, kumi na wanane. Hosa naye, wa wana wa Merari, alikuwa na wana; Shimri mkuu wao; (kwani ajapokuwa yeye si mzaliwa wa kwanza, babaye alimweka mkuu); Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu, Zekaria wa nne; wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa watu kumi na watatu. Katika hao zilikuwa zamu za mabawabu, yaani, katika hao wakuu, wenye huduma kama ndugu zao, wa kutumika katika nyumba ya BWANA. Nao wakapigiwa kura kwa ajili ya kila lango, wadogo na wakubwa kwa pamoja, kwa kufuata koo za baba zao. Kura ya lango la mashariki ikamwangukia Meshelemia. Ndipo wakamtupia kura Zekaria mwanawe, mshauri mwenye busara; na kura yake ikamtokea ya kaskazini. Ya Obed-edomu ya kusini; na ya wanawe nyumba ya akiba. Ya Shupimu na Hosa upande wa magharibi, langoni pa Shalekethi, hapo penye daraja ya kupandia, ulinzi ulifanywa kwa zamu. Upande wa mashariki walikuwapo Walawi sita, kaskazini wanne kila siku, kusini wanne kila siku, na wa nyumba ya akiba wawili wawili. Penye Parbari upande wa magharibi, walikuwapo wanne darajani, na wawili huko Parbari. Hizo ndizo zamu za mabawabu; wa wana wa Wakora, na wa wana wa Merari. Na katika Walawi; Ahia mtunzaji wa hazina ya nyumba ya Mungu, pamoja na hazina ya vitu vilivyowekwa wakfu. Wana wa Ladani; wana wa Wagershoni waliokuwa wa Ladani; wakuu wa koo za mababa waliokuwa wa Ladani, Mgershoni; Yehieli. Wana wa Yehieli; Zethamu, na Yoeli nduguye, walikuwa watunzaji wa hazina ya nyumba ya BWANA. Wa Waamrami wa Waishari, wa Wahebroni, wa Wauzieli; na Shebueli, mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, alikuwa mtunzaji wa hazina zote. Na nduguze; wa Eliezeri, Rehabia mwanawe, na Ishia mwanawe, na Yoramu mwanawe, na Zikri mwanawe, na Shelomothi mwanawe. Huyo Shelomothi na ndugu zake walikuwa wasimamizi wa hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyoviweka wakfu mfalme Daudi, na hao wakuu wa koo za mababa, na maofisa wa maelfu na wa mamia, na makamanda wa jeshi. Katika nyara zilizopatikana vitani, waliweka wakfu sehemu, ili kuitengeneza nyumba ya BWANA. Na vyote alivyoviweka wakfu Samweli mwonaji, na Sauli mwana wa Kishi, na Abneri mwana wa Neri, na Yoabu mwana wa Seruya; na mtu yeyote aliyekiweka wakfu kitu chochote, kilikuwa chini ya mkono wa Shelomothi na nduguze. Katika Waishari, Kenania na wanawe walikuwa kwa ajili ya kazi ya nje juu ya Israeli, kuwa maofisa na waamuzi. Katika Wahebroni, Hashabia na nduguze, mashujaa, elfu moja na mia saba, walikuwa na usimamizi juu ya Israeli ng'ambo ya Yordani upande wa magharibi; kwa ajili ya kazi zote za BWANA, na kwa utumishi wa mfalme. Katika Wahebroni Yeria alikuwa mkuu, yaani, wa hao Wahebroni kwa kufuata vizazi vyao kwa koo za mababa. Katika mwaka arubaini wa kutawala kwake Daudi wakatafutwa, wakaonekana huko Yazeri ya Gileadi miongoni mwao wanaume mashujaa. Na nduguze, mashujaa, walikuwa elfu mbili na mia saba, wakuu wa koo za mababa, ambao mfalme Daudi aliwaweka wawe wasimamizi juu ya Wareubeni, na Wagadi, na nusu kabila la Wamanase, kwa ajili ya kila neno lililomhusu Mungu, na kwa mambo ya mfalme.

1 Mambo ya Nyakati 26:1-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kwa zamu zao mabawabu; wa Wakora; Meshelemia mwana wa Kore, wa wana wa Ebiasafu. Naye Meshelemia alikuwa na wana; Zekaria mzaliwa wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne; Elamu wa tano, Yohana wa sita, Elioenai wa saba. Naye Obed-edomu alikuwa na wana; Shemaya mzaliwa wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, na Sakari wa nne, na Nethaneli wa tano; Amieli wa sita, Isakari wa saba, Peulethai wa nane; kwa jinsi Mungu alivyombariki. Naye mwanawe Shemaya akazaliwa wana, waliomiliki juu ya mbari ya baba yao; kwa kuwa walikuwa waume mashujaa. Wana wa Shemaya; Othni, na Refaeli, na Obedi, na Elzabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu, na Semakia. Hao wote walikuwa wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, watu hodari wawezao huo utumishi; watu wa Obed-edomu sitini na wawili. Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze, watu mashujaa, kumi na wanane. Hosa naye, wa wana wa Merari, alikuwa na wana; Shimri mkuu wao; (kwani ajapokuwa yeye si mzaliwa wa kwanza, babaye alimweka mkuu); Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu, Zekaria wa nne; wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa watu kumi na watatu. Katika hao zilikuwa zamu za mabawabu, yaani, katika hao wakuu, wenye ulinzi sawasawa na ndugu zao, wa kutumika katika nyumba ya BWANA. Nao wakatupiwa kura kwa ajili ya kila lango, wadogo sawasawa na wakubwa, kwa kadiri ya mbari za baba zao. Kura ya mashariki ya lango ikamwangukia Meshelemia. Ndipo wakamtupia kura Zekaria mwanawe, mshauri mwenye busara; na kura yake ikamtokea ya kaskazini. Ya Obed-edomu ya kusini; na ya wanawe nyumba ya akiba. Ya Shupimu na Hosa upande wa magharibi, langoni pa Shalekethi, hapo penye daraja ya kupandia, ulinzi kwa ulinzi. Upande wa mashariki walikuwapo Walawi sita, kaskazini wanne kila siku, kusini wanne kila siku, na wa nyumba ya akiba wawili wawili. Penye Parbari upande wa magharibi, walikuwapo wanne darajani, na wawili huko Parbari. Hizo ndizo zamu za mabawabu; wa wana wa Wakora, na wa wana wa Merari. Na katika Walawi; Ahia alikuwa juu ya hazina za nyumba ya Mungu, na juu ya hazina za vitu vilivyowekwa wakfu. Wana wa Ladani; wana wa Wagershoni waliokuwa wa Ladani; wakuu wa mbari za mababa waliokuwa wa Ladani, Mgershoni; Yehieli. Wana wa Yehieli; Zethamu, na Yoeli nduguye, juu ya hazina za nyumba ya BWANA. Wa Waamramu, wa Waishari, wa Wahebroni, wa Wauzieli; na Shebueli, mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, alikuwa mtawala hazina zote. Na nduguze; wa Eliezeri, Rehabia mwanawe, na Ishia mwanawe, na Yoramu mwanawe, na Zikri mwanawe, na Shelomothi mwanawe. Huyo Shelomothi na ndugu zake walikuwa juu ya hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyoviweka wakfu mfalme Daudi, na hao wakuu wa mbari za mababa, na maakida wa maelfu na wa mamia, na maakida wa jeshi. Katika nyara zilizopatikana vitani, waliweka wakfu sehemu, ili kuitengeneza nyumba ya BWANA. Na vyote alivyoviweka wakfu Samweli mwonaji, na Sauli mwana wa Kishi, na Abneri mwana wa Neri, na Yoabu mwana wa Seruya; na mtu ye yote aliyekiweka wakfu kitu cho chote, kilikuwa chini ya mkono wa Shelomothi na nduguze. Katika Waishari, Kenania na wanawe walikuwa kwa ajili ya kazi ya nje juu ya Israeli, kuwa maakida na makadhi. Katika Wahebroni, Hashabia na nduguze, mashujaa, elfu na mia saba, walikuwa na usimamizi juu ya Israeli ng’ambo ya Yordani upande wa magharibi; kwa ajili ya kazi zote za BWANA, na kwa utumishi wa mfalme. Katika Wahebroni Yeria alikuwa mkuu, yaani, wa hao Wahebroni kwa kufuata vizazi vyao kwa mbari za mababa. Katika mwaka arobaini wa kutawala kwake Daudi wakatafutwa, wakaonekana huko Yazeri ya Gileadi miongoni mwao waume mashujaa. Na nduguze, mashujaa, walikuwa elfu mbili na mia saba, wakuu wa mbari za mababa, ambao mfalme Daudi aliwaweka wawe wasimamizi juu ya Wareubeni, na Wagadi, na nusu kabila ya Wamanase, kwa ajili ya kila neno lililomhusu Mungu, na kwa mambo ya mfalme.

1 Mambo ya Nyakati 26:1-32 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hii ndiyo migawanyo ya mabawabu: Kutoka kwa wana wa Kora alikuwa: Meshelemia mwana wa Kore, mmoja wa wana wa Asafu. Meshelemia alikuwa na wana wafuatao: Zekaria mzaliwa wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne, Elamu wa tano Yehohanani wa sita na Eliehoenai wa saba. Obed-Edomu naye alikuwa na wana wafuatao: Shemaya mzaliwa wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, Sakari wa nne, Nethaneli wa tano, Amieli wa sita, Isakari wa saba, na Peulethai wa nane. (Kwa kuwa Mungu alikuwa amembariki Obed-Edomu.) Shemaya mwanawe pia alikuwa na wana, waliokuwa viongozi katika jamaa ya baba yao kwa sababu walikuwa watu wenye uwezo mkubwa. Wana wa Shemaya ni: Othni, Refaeli, Obedi na Elizabadi; jamaa zake Elihu na Semakia walikuwa pia watu wenye uwezo. Hawa wote walikuwa wazao wa Obed-Edomu; wao na wana wao na jamaa zao walikuwa watu wenye uwezo pamoja na nguvu za kufanya kazi. Wazao wa Obed-Edomu jumla yao walikuwa sitini na wawili. Meshelemia alikuwa na wana na jamaa zake, waliokuwa watu wenye uwezo: jumla yao watu kumi na wanane. Hosa, Mmerari, alikuwa na wana wafuatao: Shimri alikuwa mkuu wao (baba yake alikuwa amemweka yeye kuwa mkuu ijapokuwa hakuwa mzaliwa wa kwanza), Hilkia wa pili, Tabalia wa tatu na Zekaria wa nne. Wana na jamaa za Hosa jumla yao walikuwa watu kumi na watatu. Hii migawanyo ya mabawabu, kupitia wakuu wao, walikuwa na zamu za kuhudumu hekaluni mwa BWANA kama jamaa zao walivyokuwa nazo. Kura zilipigwa kwa kila lango, kufuatana na jamaa zao, wakubwa kwa wadogo. Kura ya Lango la Mashariki ilimwangukia Shelemia. Kisha wakapiga kura kwa Zekaria mwanawe, aliyekuwa mshauri mwenye hekima, nayo kura ya Lango la Kaskazini ikamwangukia. Kura ya Lango la Kusini ikamwangukia Obed-Edomu, nayo kura ya maghala ikawaangukia wanawe. Kura za Lango la Magharibi na Lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu zikawaangukia Shupimu na Hosa. Zamu za walinzi ziligawanywa kwa usawa: Kulikuwa na Walawi sita kila siku upande wa mashariki, wanne upande wa kaskazini, wanne upande wa kusini, na wawili wawili kwa mara moja kwenye ghala. Kuhusu ukumbi kuelekea magharibi, kulikuwa na wanne barabarani na wawili kwenye ukumbi wenyewe. Hii ndiyo iliyokuwa migawanyo ya mabawabu waliokuwa wazao wa Kora na wa Merari. Katika Walawi, Ahiya alikuwa mwangalizi wa hazina za nyumba ya Mungu na mwangalizi wa hazina za vitu vilivyowekwa wakfu. Wazao wa Ladani, waliokuwa Wagershoni kupitia Ladani na waliokuwa viongozi wa jamaa za Ladani Mgershoni, walikuwa Yehieli, wana wa Yehieli, wana wa Zethamu na wa nduguye Yoeli. Wao walikuwa waangalizi wa hazina za Hekalu la BWANA. Kutoka kwa wana wa Amramu, wana wa Ishari, wana wa Hebroni na wana wa Uzieli: Shebueli, mzao wa Gershomu mwana wa Mose, alikuwa afisa mwangalizi wa hazina. Jamaa zake kutoka kwa Eliezeri, wanawe walikuwa: Rehabia, Yeshaya, Yoramu, Zikri na Shelomithi. Shelomithi na jamaa zake walikuwa waangalizi wa hazina zote za vitu vile vilivyowekwa wakfu na Mfalme Daudi, kwa viongozi wa jamaa waliokuwa majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, na kwa maafisa wengine wa jeshi. Baadhi ya nyara zilizotekwa vitani waliziweka wakfu kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu la BWANA. Kila kitu kilichokuwa kimewekwa wakfu na Samweli mwonaji, na Sauli mwana wa Kishi, Abneri mwana wa Neri, na Yoabu mwana wa Seruya, pamoja na vitu vingine vyote vilivyokuwa vimewekwa wakfu, vyote vilikuwa chini ya uangalizi wa Shelomithi na jamaa zake. Kutoka kwa wana wa Ishari: Kenania na wanawe walipewa kazi nje ya Hekalu kama maafisa na waamuzi juu ya Israeli. Kutoka kwa wana wa Hebroni: Hashabia na jamaa zake, watu 1,700 wenye uwezo, waliwajibika katika Israeli magharibi ya Yordani kwa ajili ya kazi zote za BWANA na utumishi wa mfalme. Kuhusu wana wa Hebroni, Yeria alikuwa mkuu wao kufuatana na orodha ya jamaa yao. Katika mwaka wa arobaini wa utawala wa Daudi uchunguzi ulifanyika katika kumbukumbu, nao watu wenye uwezo miongoni mwa wana wa Hebroni wakapatikana huko Yazeri katika Gileadi. Yeria alikuwa na jamaa ya watu 2,700 waliokuwa watu wenye uwezo na viongozi wa jamaa, naye Mfalme Daudi akawaweka kuangalia Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila Manase kuhusu kila jambo lililomhusu Mungu na shughuli za mfalme.