Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 17:16-27

1 Mambo ya Nyakati 17:16-27 SRUV

Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za BWANA; akasema Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumishi wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia kama mtu mwenye cheo, Ee BWANA Mungu. Na Daudi akuambie nini tena zaidi kwa habari ya heshima aliyotendewa mtumishi wako? Kwa maana wewe umemjua mtumishi wako. Ee BWANA, kwa ajili ya mtumishi wako, na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Ee BWANA, hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake mwenyewe, ili wawe watu wake, na kujifanyia jina kwa njia ya mambo makuu, yenye kuogofya, kwa kufukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri? Kwa maana watu wako Israeli ndio uliowafanya kuwa watu wako wa milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA, neno lile ulilolinena kuhusu mtumishi wako, na kuhusu nyumba yake, na lifanywe imara milele, ukafanye kama ulivyosema. Jina lako na liwe imara, likatukuzwe milele, kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu wa Israeli, naam, Mungu juu ya Israeli; na hiyo nyumba ya Daudi mtumwa wako imefanywa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, Ee Mungu wangu, umenifunulia mimi mtumishi wako ya kuwa utanijengea nyumba; kwa hiyo mimi mtumishi wako nimeona vema moyoni mwangu kuomba mbele yako. Na sasa, Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu, nawe umemwahidia mtumishi wako jambo hili jema; nawe sasa umekuwa radhi kuibarikia nyumba ya mtumishi wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, BWANA, umebarikia, nayo imebarikiwa milele.