Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nya 17:16-27

1 Nya 17:16-27 SUV

Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za BWANA; akasema Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia sawasawa na hali ya mtu mwenye cheo, Ee BWANA Mungu. Na Daudi akuambie nini tena zaidi kwa habari ya heshima aliyotendewa mtumwa wako? Kwa maana wewe umemjua mtumwa wako. Ee BWANA, kwa ajili ya mtumwa wako, na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Ee BWANA, hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake mwenyewe, ili wawe watu wake, na kujifanyia jina kwa njia ya mambo makuu, yenye kuogofya, kwa kufukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri? Kwa maana watu wako Israeli ndio uliowafanya kuwa watu wako wa milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yake, na lifanywe imara milele, ukafanye kama ulivyosema. Jina lako na liwe imara, likatukuzwe milele, kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu wa Israeli, naam, Mungu juu ya Israeli; na hiyo nyumba ya Daudi mtumwa wako imefanywa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, Ee Mungu wangu, umenifunulia mimi mtumwa wako ya kuwa utanijengea nyumba; kwa hiyo mimi mtumwa wako nimeona vema moyoni mwangu kuomba mbele yako. Na sasa, Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema; nawe sasa umekuwa radhi kuibarikia nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, BWANA, umebarikia, nayo imebarikiwa milele.

Soma 1 Nya 17

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha