Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 17:16-27

1 Mambo ya Nyakati 17:16-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha mfalme Daudi akaingia ndani ya hema na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu akaomba, “Mimi ni nani, ee Mwenyezi-Mungu, na nyumba yangu ni nini hata unitukuze hivi? Isitoshe, umenifanyia mengine zaidi: Umenitolea ahadi juu ya vizazi vyangu vijavyo ee Mwenyezi-Mungu! Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi mtumishi wako, kwa kunitukuza hivyo? Wewe unanijua mimi mtumishi wako. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa kufuatana na moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Hakuna mwingine kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu, na yote tunayoyasikia yanathibitisha kwamba hakuna Mungu mwingine ila wewe. Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kulinganishwa na watu wako wa Israeli ambao peke yao Mungu wao alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ulijifanyia jina kwa kutenda mambo makubwa na ya ajabu hapo ulipoyafukuza mataifa mbele ya watu wako ambao uliwakomboa kutoka Misri. Hata umejifanyia watu wako wa Israeli kuwa watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu, umekuwa Mungu wao. “Basi sasa, ewe Mwenyezi-Mungu, liimarishe milele neno lako ulilosema kunihusu mimi mtumishi wako na kuhusu jamaa yangu. Nalo jina lako litatukuzwa milele, nao watu watasema, ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, ndiye Mungu wa Israeli!’ Na jamaa yangu, mimi Daudi mtumishi wako, itaimarika mbele yako. Maana ee Mungu wangu nimepata ujasiri kukuomba kwa sababu wewe, umenifunulia ukisema ya kwamba utanijengea nyumba. Sasa ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe Mungu, umeniahidi mimi mtumishi wako jambo hili jema; kwa hiyo nakuomba uibariki nyumba yangu, mimi mtumishi wako, ili idumu milele mbele yako; kwani unachobariki wewe, huwa kimebarikiwa milele.”

1 Mambo ya Nyakati 17:16-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za BWANA; akasema Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumishi wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia kama mtu mwenye cheo, Ee BWANA Mungu. Na Daudi akuambie nini tena zaidi kwa habari ya heshima aliyotendewa mtumishi wako? Kwa maana wewe umemjua mtumishi wako. Ee BWANA, kwa ajili ya mtumishi wako, na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Ee BWANA, hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake mwenyewe, ili wawe watu wake, na kujifanyia jina kwa njia ya mambo makuu, yenye kuogofya, kwa kufukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri? Kwa maana watu wako Israeli ndio uliowafanya kuwa watu wako wa milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA, neno lile ulilolinena kuhusu mtumishi wako, na kuhusu nyumba yake, na lifanywe imara milele, ukafanye kama ulivyosema. Jina lako na liwe imara, likatukuzwe milele, kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu wa Israeli, naam, Mungu juu ya Israeli; na hiyo nyumba ya Daudi mtumwa wako imefanywa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, Ee Mungu wangu, umenifunulia mimi mtumishi wako ya kuwa utanijengea nyumba; kwa hiyo mimi mtumishi wako nimeona vema moyoni mwangu kuomba mbele yako. Na sasa, Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu, nawe umemwahidia mtumishi wako jambo hili jema; nawe sasa umekuwa radhi kuibarikia nyumba ya mtumishi wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, BWANA, umebarikia, nayo imebarikiwa milele.

1 Mambo ya Nyakati 17:16-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za BWANA; akasema Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia sawasawa na hali ya mtu mwenye cheo, Ee BWANA Mungu. Na Daudi akuambie nini tena zaidi kwa habari ya heshima aliyotendewa mtumwa wako? Kwa maana wewe umemjua mtumwa wako. Ee BWANA, kwa ajili ya mtumwa wako, na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Ee BWANA, hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake mwenyewe, ili wawe watu wake, na kujifanyia jina kwa njia ya mambo makuu, yenye kuogofya, kwa kufukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri? Kwa maana watu wako Israeli ndio uliowafanya kuwa watu wako wa milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yake, na lifanywe imara milele, ukafanye kama ulivyosema. Jina lako na liwe imara, likatukuzwe milele, kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu wa Israeli, naam, Mungu juu ya Israeli; na hiyo nyumba ya Daudi mtumwa wako imefanywa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, Ee Mungu wangu, umenifunulia mimi mtumwa wako ya kuwa utanijengea nyumba; kwa hiyo mimi mtumwa wako nimeona vema moyoni mwangu kuomba mbele yako. Na sasa, Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema; nawe sasa umekuwa radhi kuibarikia nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, BWANA, umebarikia, nayo imebarikiwa milele.

1 Mambo ya Nyakati 17:16-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za BWANA, akasema: “Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo? Kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Mungu, umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukuka kuliko watu wote, Ee BWANA Mungu. “Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako, Ee BWANA Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa sana na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kubwa sana. “Hakuna aliye kama wewe, Ee BWANA Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe. Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee BWANA Mungu, umekuwa Mungu wao. “Sasa basi, BWANA ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi, ili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako. “Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea yeye nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. Basi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele machoni pako; kwa ajili yako, Ee BWANA, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”