1 Mambo ya Nyakati 16:4-22
1 Mambo ya Nyakati 16:4-22 SRUV
Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la BWANA, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, BWANA, Mungu wa Israeli; Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Metithia, na Eliabu, na Benaya, na Obed-edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi; nao makuhani Benaya na Yahazieli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la Agano la Mungu. Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru BWANA, kwa mkono wa Asafu na nduguze. Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni nyimbo za kumsifu; Yatangazeni matendo yake yote ya ajabu. Jisifuni kwa jina lake takatifu; Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA. Mtafuteni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote. Yakumbukeni matendo yake yote ya ajabu aliyoyafanya; Miujiza yake na hukumu za kinywa chake; Enyi wazao wa Israeli, mtumishi wake, Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Duniani kote kuna hukumu zake. Likumbukeni agano lake milele, Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Abrahamu, Na kiapo chake kwa Isaka; Aliyomthibitishia Yakobo kuwa amri, Na kwa Israeli kuwa agano la milele. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa; Mlipokuwa watu wawezao kuhesabiwa; Naam, watu wachache na wageni ndani yake. Mkitangatanga toka taifa hadi taifa, Toka ufalme mmoja hadi kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee; Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao; Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.