1 Nya 16:4-22
1 Nya 16:4-22 SUV
Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la BWANA, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, BWANA, Mungu wa Israeli; Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Matithiya, na Eliabu, na Benaya, na Obed-edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi; nao makuhani Benaya na Yahazieli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la agano la Mungu. Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru BWANA, kwa mkono wa Asafu na nduguze. Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi; Zitafakarini ajabu zake zote. Jisifuni kwa jina lake takatifu; Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA. Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote. Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya; Miujiza yake na hukumu za kinywa chake; Enyi wazao wa Israeli, mtumishi wake, Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake. Likumbukeni agano lake milele, Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka; Alilomthibitishia Yakobo kuwa amri, Na Israeli liwe agano la milele. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa; Mlipokuwa watu wawezao kuhesabiwa; Naam, watu wachache na wageni ndani yake. Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee; Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao; Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.