Zab 69:16-36
Zab 69:16-36 SUV
Ee BWANA, unijibu, maana fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee. Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi. Uikaribie nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie. Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote. Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu. Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. Meza yao mbele yao na iwe mtego; Naam, wakiwa salama na iwe tanzi. Macho yao yatiwe giza wasione, Na viuno vyao uvitetemeshe daima. Uimwage ghadhabu yako juu yao, Na ukali wa hasira yako uwapate. Matuo yao na yawe ukiwa, Pasiwe na mtu wa kukaa hemani mwao. Maana wanamwudhi mtu uliyempiga Wewe, Wanasimulia maumivu ya hao uliowatia jeraha. Uwaongezee uovu juu ya uovu, Wala wasiingie katika haki yako. Na wafutwe katika chuo cha uhai, Wala pamoja na wenye haki wasiandikwe. Nami niliye maskini na mtu wa huzuni, Mungu, wokovu wako utaniinua. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, Nami nitamtukuza kwa shukrani. Nayo yatampendeza BWANA kuliko ng’ombe, Au ndama mwenye pembe na kwato. Walioonewa watakapoona watafurahi; Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe. Kwa kuwa BWANA huwasikia wahitaji, Wala hawadharau wafungwa wake. Mbingu na nchi zimsifu, Bahari na vyote viendavyo ndani yake. Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda, Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki. Wazao wa watumishi wake watairithi, Nao walipendao jina lake watakaa humo.