Zaburi 69:16-36
Zaburi 69:16-36 BHN
Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu, kwa wema na fadhili zako; unielekee kwa wingi wa huruma yako. Usimfiche mtumishi wako uso wako; unijibu haraka, maana niko hatarini. Unijie karibu na kunikomboa, uniokoe na maadui zangu wengi. Wewe wajua ninavyotukanwa, wajua aibu na kashfa ninazopata; na maadui zangu wote wewe wawajua. Kashfa zimeuvunja moyo wangu, nami nimekata tamaa. Nimetafuta kitulizo lakini sikupata, wa kunifariji lakini sikumpata. Walinipa sumu kuwa chakula, na nilipokuwa na kiu wakanipa siki. Karamu zao na ziwe mtego kwao, na sikukuu zao za sadaka ziwanase. Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona, uitetemeshe daima migongo yao. Uwamwagie hasira yako, ghadhabu yako iwakumbe. Kambi zao ziachwe mahame, asiishi yeyote katika mahema yao. Maana wanawatesa wale uliowaadhibu, wanawaongezea majeraha wale uliowajeruhi. Uwaadhibu kwa kila uovu wao; uwakatalie kabisa msamaha wako. Uwafute katika kitabu cha walio hai, wasiwemo katika orodha ya waadilifu. Lakini mimi mnyonge na mgonjwa; uniinue juu, ee Mungu, uniokoe. Kwa wimbo nitalisifu jina la Mungu, nitamtukuza kwa shukrani. Jambo hili litampendeza Mwenyezi-Mungu zaidi, kuliko kumtolea tambiko ya ng'ombe, kuliko kumtolea fahali mzimamzima. Wanyonge wataona hayo na kufurahi; wanaomheshimu Mungu watapata moyo. Mwenyezi-Mungu huwasikiliza fukara; hatawasahau kamwe watu wake wafungwa. Enyi mbingu na dunia msifuni Mungu; bahari na vyote vilivyomo, msifuni. Maana Mungu atauokoa mji Siyoni, na kuijenga tena miji ya Yuda. Watu wake wataishi humo na kuimiliki; wazawa wa watumishi wake watairithi, wale wanaopenda jina lake wataishi humo.